Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo tarehe 19 Septemba, 2023 ameendelea na ziara yake katika Wilaya ya Bunda ambapo amekagua na kushiriki ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mara inayojengwa katika eneo la Bulamba, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mtanda ameshiriki kuchimba kifusi na kujaza kifusi katika baadhi ya majengo yanayoendelea kujengwa katika eneo hilo na kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri na Ofisi ya Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu Mkoa wa Mara kufuatilia kwa ukaribu ujenzi wa shule hiyo.
“Wenzetu mikoa mingine shule hizi zimekamilika lakini kutokana na changamoto zilizokuwepo bado ujenzi wa shule hii unaendelea, niwaombe tuongeze kasi ya ujenzi wa shule hii” amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, Mhe. Mtanda amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kumchukulia hatua mtumishi wa kitengo cha manunuzi ambaye hakuonekana ofisini kwa muda wa miezi mitatu bila kupewa ruhusa na mwajiri.
Mhe. Mtanda amewaagiza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia utekelezaji wa miradi ili kuikamilisha kwa kutumia fedha zinazoletwa na Serikali badala ya kutafuta nyongeza au kutumia fedha za mapato ya ndani katika miradi hiyo.
Mheshimiwa Mtanda pia amewataka Maafisa Elimu wa Halmashauri na Waganga Wakuu wa Halmashauri kufuatilia kwaukaribu miradi ya sekta zao inapokuwa inatekelezwa.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa alitembelea mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda na Sekondari ya Bunda Stoo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mara, Shule ya Sekondari Sunsi, Shule ya Sekondari kasuguti zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bunda na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Bunda, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya, wawakilishi wa Makatibu Tawala Wasaidizi sehemu za Elimu na Miundombinu, wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, wakuu wa taasisi za umma, baadhi ya watumishi wa Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa