Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo tarehe 31 Oktoba, 2023 ametembelea Shule ya Msingi Ikorongo iliyopo katika Wilaya ya Serengeti na kumpongeza Mwalimu Yusuf Pangoma kwa ubunifu wake katika ufundishaji.
Mhe. Mtanda amesema hayo baada yeye na watu alioambatana naye kwenye ziara yake kushuhudia mwalimu Pangoma akiwa darasani akiwafundisha wanafunzi wa darasa la kwanza wa shule hiyo.
“Awali nilimuona huyu Mwalimu akifundisha kwenye mitandao ya kijamii nikafurahishwa naye na nikamuomba aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Ally Salum Hapi aje kumtembelea” amesema Mtanda.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa aliendelea kuwasiliana na Mwalimu Pangoma na alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara akaamua kwenda kumtembelea ili kumtia moyo katika kazi nzuri anayoifanya katika shule hiyo.
Mhe. Mtanda alitoa zawadi ya shilingi 200,000 kwa Mwalimu Pangoma, shilingi 100,000 kwa ajili ya chai ya walimu wa shule hiyo na kuahidi mifuko 100 ya simenti kwa ajili ya kukarabati majengo ya shule hiyo.
Mhe. Mtanda pia ameahidi kuliomba Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kutoa madawati kwa ajili ya kupunguza uhaba wa madawati katika shule hiyo baada ya kushuhudia wanafunzi wengi wakikaa kwenye dawati moja.
Mkuu wa Mkoa pia alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kukamilisha darasa moja lililojengwa kwa nguvu za wananchi na kukarabati madarasa ya shule hiyo ili kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.
Aidha, Mhe. Mtanda amewataka walimu wa hiyo na watumishi wote kwa ujumla kujiendeleza kimasomo na kuchapa kazi kwa bidii ili waweze kujijenga zaidi katika maisha yao bila kujali sehemu wanapofanyia kazi.
“Haya mazingira ya kijijini yanaweza kuwa fursa kubwa kwako kama ukiamua kuyakubali na kufanya kazi kwa bidii na kujishughulisha na kilimo au ufugaji jambo ambalo aliyepo mjini hawezi kulifanya” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda pia aliwapongeza walimu wa shule hiyo kwa ufaulu mzuri wa wanafunzi katika mitihani ya darasa la saba kwa miaka minne mfululizo na kuwataka waendelee na ufaulu huo.
Katika kuunga mkono juhudi za ukarabati wa shule hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji aliahidi kutoa sementi mifuko 50 kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo.
Wakati huo huo, Mhe. Said Mtanda amewataka wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao wanaosoma katika shule mbalimbali ili kuweza kubaini mahudhurio ya wanafunzi na kama kuna tatizo mapema waweze kurekebisha.
Akizungumza na wazazi waliohudhuria kikao katika Shule ya Sekondari ya Morotonga, Mhe. Mtanda amesema bila wazazi kutoa ushirikiano kwa walimu, walimu peke yao hawawezi kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi.
Amewapongeza wazazi hao kwa kuhudhuria na kuwakemea wazazi ambao waliitwa na hawakuhudhuria kikao hicho.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti, viongozi, Mkurugenzi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa