Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohammed Mtanda leo amefanya ziara katika Wilaya ya Tarime na kumtaka Mkandarasi wa Soko la kimkakati la Halmashauri wa Mji wa Tarime kukamilisha mradi huo kwa mujibu wa mkataba tarehe 18 Novemba, 2023.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa Serikali imeleta pesa yote ya utekeleaji wa mradi huo hata hivyo Mkandarasi wa mradi huo Mohammed Builders Limited ndie anayechelewesha ukamilishaji wa mradi huo huku wananchi wakisubiria huduma.
“Mkandarasi aagizwe kuongeza watumishi na aanze kukamilisha kazi za nje na maduka ya nje ya soko hili ili yaanze kutoa huduma kwa wananchi na hamna muda utakaoongezwa tena katika mkataba wake” amesema Mhe. Mtanda.
Aidha amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri wa ya Mji wa Tarime kutenga maeneo ya wafanyabiashara wadogo, pikipiki na bajaji na mama/baba lishe katika soko hilo ili wateja wa hali zote waweze kuhudumiwa na soko hilo.
Aidha, amemuagiza Mhandisi Mshauri kuwasilisha ofisini kwake nakala ya ushauri na mapendekezo aliyoyatoa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kuhusiana na ujenzi wa soko hilo.
Mhe. Mtanda amezitaka Halmashauri nyingine za Mji wa Bunda na Manispaa ya Musoma kuiga ubunifu wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa uwekezaji huo ambao amesema utawanufaisha wananchi na wafanyabiashara wa Mji wa Tarime.
Akitoa taarifa ya mradi, Mhandisi Mshauri Eng. Leonard Mwangoka ameeleza kuwa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 9.5 ulipangwa kukamilika ndani ya miezi 15 kuanzia tarehe 19 Januari, 2022 hadi tarehe 19 Aprili, 2023 hata hivyo Mkandarasi ameongezewa muda hadi tarehe 18 Novemba, 2023.
Eng. Mwangoka ameeleza kuwa mradi kwa sasa upo katika hatua ya ukamilishaji wa mradi huo na ujenzi unaendelea vizuri na unakadiriwa kufikia asilimia 84 ya utekelezaji wake.
“Kazi zinazoendelea ni ujenzi wa terrazzo katika maeneo ya vizimba na kolido zote, plasta baadhi ya maeneo, upakaji wa rangikatika maduka ya nje, kuweka milango kwenye maduka, uwekaji wa vizingiti vya chuma kwenye kolido na kuweka bodi za umeme kwenye maduka” amesema Mhandisi Mwangoka.
Bwana Mwangoka ameeleza kuwa mpaka sasa Mkandarasi wa mradi huo ameshalipwa zaidi ya shilingi 4.7 ambayo ni sawa na asilimia 49.9 ya malipo yote anayotakiwa kulipwa na kwa sasa malipo yaliyopo kwa mwajiri ni shilingi milioni moja tu.
Kwa mujibu wa Eng. Mwangoka, hadi kufikia tarehe 23 Oktoba, 2023 mradi huo umetoa ajira kwa watu 441 na utakapokamilika utakuwa na maduka ya nje 134, maduka ya ndani 188, vizimba 160, bucha 3, migahawa 2, supamaketi 1 na benki 2.
Akiwa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, Mkuu wa Mkoa alitembelea pia mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Nyagisese na kupongeza Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kazi nzuri iliyofanyika katika ujenzi wa shule hiyo.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, baadhi ya maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, baadhi ya viongozi na wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa