Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amekabidhi magari matano ya usimamizi wa Sekta ya Afya na kuwataka viongozi na wasimamizi wa sekta ya afya kuhakikisha magari hayo yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo, Mhe. Mtanda amewataka viongozi na watendaji wa Mkoa na Halmashauri kuhakikisha magari hayo yanatunzwa kwa mujibu wa taratibu za Serikali na yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuboresha huduma za sekta ya afya Mkoa wa Mara.
“Sitarajii kuona magari haya yakitumika kubeba mizigo mizito na mikaa, haya ni magari ya usimamizi na yatumike kufanya shughuli za usimamizi katika sekta ya afya” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda pia amewataka wasimamizi wa magari hayo kuangalia mienendo ya madereva wao ili kujiridhisha na uendeshaji salama wa magari ya Serikali kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Aidha, Mhe. Mtanda amewakumbusha viongozi kuhusu maelekezo aliyoyatoa awali kuhusu utengenezaji wa magari ya Serikali ili yaweze kutoa huduma zilizokusudiwa.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu ameeleza kuwa magari hayo matano yanayokabidhiwa ni sehemu ya magari 33 ya sekta ya afya yaliyotolewa na Serikali kwa Mkoa wa Mara katika mwaka huu wa fedha.
“Kwa sasa tunasubiri magari ya usimamizi ya Halmashauri tano ambayo bado hayajapokelewa na yanatarajiwa kupokelewa wakati wowote kuanzia sasa” amesema Dkt. Masatu.
Dkt. Masatu ameeleza kuwa tayari baadhi ya magari ikiwa ni pamoja na magari ya kubeba wagonjwa kwa ajili ya Halmashauri zote za Mkoa wa Mara na Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere yamepokelewa na kukabidhiwa kwa walengwa.
Halmashauri zilizokabidhiwa magari ya usimamizi wa sekta ya afya leo ni Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Dkt. Masatu ameeleza kuwa magari hayo yataboresha ukaguzi na usimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya na kuwawezesha wasimamizi wa sekta ya afya ngazi za Halmashauri na Mkoa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Magari 33 yametolewa na Serikali kwa ajili ya Usimamizi wa sekta ya Afya magari 13, kwa ajili ya Mkoa, Halmashauri, Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo cha Maafisa Tabibu Musoma na magari ya kubeba wagonjwa 20 kwa ajili ya Halmashauri tisa na Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa).
Hafla ya kukabidhi magari imehudhuriwa pia na Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wasaidizi na Wakuu wa Vitengo vya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Wakurugenzi wa Halmashauri na baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa