Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao cha viongozi na watendaji wa Mkoa wa Mara kuhusu utoaji wa chakula shuleni na kuwataka viongozi, wazazi na wadau wote kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wa Mkoa wa Mara wanapata chakula cha mchana shuleni kuanzia Januari, 2025.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza katika kikao hicho na kuwataka viongozi wa Serikali wa Mkoa wa Mara kusimamia maelekezo hayo na kuhakikisha wanafunzi wote wanapata angalau mlo wa mmoja wa mchana wakiwa shuleni ili waweze kujifunza vizuri.
“Haikubaliki kuendelea kuwafanyia ukatili wanafunzi kwa kuwashindisha na njaa kwa sababu tu viongozi na wazazi tumeshindwa kutimiza wajibu wetu katika kutoa chakula shuleni” amesema Mhe. Mtambi na kuwataka wazazi na walezi wote kuchangia ili wanafunzi wapate chakula shuleni.
Mhe. Mtambi amesema chakula kinachochangiwa sio cha ziada bali ni chakula ambacho mtoto akiwa nyumbani angekula na hivyo ni wajibu wa wazazi na walezi wa wanafunzi kutoa chakula hicho ili wanafunzi wapate chakula wakiwa shuleni.
Kanali Mtambi amezitaka Halmashauri kuhakikisha kuwa shule zote zenye maeneo au mashamba zitumie maeneo hayo kulipa na kupata chakula ili kuwasaidia wazazi katika mchango wa chakula na kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo kuhusu kilimo na shughuli za kujitegemea.
Mhe. Mtambi amewataka wadau wa elimu kuchangia kwa hali na mali ili kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chakula shuleni na Halmashauri kutunga sheria ndogo za kusimamia utoaji wa chakula shuleni ili wazazi/walezi wanaokaidi kuchangia wachukuliwe hatua za kisheria.
Mhe. Mtambi amezitaka Halmashauri kuhakikisha kuwa chakula kinachochangwa na wazazi kinahifadhiwa vizuri na kwa usalama katika maeneo ya shule na kushughulikia wasiwasi wa wananchi kuwa chakula kinachochangwa kinatumika vibaya na walimu.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bi. Judith Mrimi amesema programu ya chakula shuleni ni muhimu kwa ajili ya kuongeza udahili na usajili wa wanafunzi, mahudhurio, usikivu na kuinua ufaulu wa wanafunzi katika mitihani.
Bibi Mrimi amesema kwa mujibu wa mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa wanafunzi wa Elimumsingi, wanafunzi wote wa shule za kutwa za msingi na sekondari wanapaswa kupata huduma ya chakula cha mchana shuleni.
Bibi Mrimi amesema mwongozo huo umebainisha kuwa chakula kwa ajili ya wanafunzi kitapatikana kutoka kwa Serikali kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na kwa shule za kutwa michango ya chakula itatoka kwa wadau wa elimu, sekta binafsi, wabia wa maendeleo, mashamba na bustani za shule, michango ya wazazi.
Bi Mrimi amesema kuwa mwongozo huo umeainisha michango ya chakula shuleni inaweza kuwa ni pamoja na michango ya vyakula, fedha taslimu, nguvu kazi, miundombinu na michango ya uwezeshaji au kuwajengea wananchi uwezo wa kitaalamu.
Bibi Mrimi amesema Halmashauri ni moja ya wadau muhimu wa utoaji wa chakula shuleni na inatakiwa kuweka kwenye mipango yake shughuli za kuhamasisha wazazi na jamii kupitia viongozi wa mitaa au vijiji kushiriki utoaji wa chakula shuleni, udhibiti wa ubora na usalama wa chakula kwa kutoa elimu na kuandaa sheria ndogondogo za utoaji wa chakula shuleni.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa