Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameshiriki Kongamano la Pili la Kisayansi kuhusu ikolojia ya bonde la Mto Mara katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara, Narok nchini Kenya na kuwataka wadau kutekeleza maazimio yaliyofikiwa katika Kongamano la kwanza lililofanyika katika Mji wa Mugumu wilaya ya Serengeti, Tanzania tarehe 14 Septemba, 2023.
Mhe. Mtambi ameeleza kuwa pamoja na ukweli kuwa maazimio hayo yalikuwa mazuri lakini yasipotekelezwa hayawezi kusaidia katika kulinda ikolojia ya Bonde la Mto Mara na kuleta manufaa yaliyotarajiwa kwa wananchi wanaotegemea bonde la Mto Mara katika maisha yao ya kila siku.
“Wakati sasa umefika wa kwenda mbali zaidi ya majadiliano na kugeuza ujuzi, maarifa na maazimio tuliyoyapata katika kongamano la kwanza kuwa hatua muhimu katika utekelezaji wa maazimio hayo ili kupata manufaa yanayotarajiwa” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuchukua hatua mbalimbali kulinda mazingira ya bonde la Mto Mara ili kulinda ikolojia ya bonde hilo kwa manufaa yetu na wanyama kutoka wanaotegemea bonde hilo.
Mhe. Mtambi amesema, kongamano hili ni muhimu katika maadhimisho ya Siku ya Mara kwa sababu ni jukwaa muhimu la kusikiliza mawasilisho mbalimbali yanayoongelea lengo kuu la maadhimisho hayo ambalo ni kuimarisha ushirikiano wa wananchi, viongozi, wataalamu na wanasayansi katika kusimamia uhifadhi na ikolojia ya bonde la Mto Mara.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Msemaji Mkuu wa Kongamano hilo Prof. Patrice Lumumba kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya amesema katika kongamano zima ni tafsiri ya kauli mbiu tu ndio imewekwa kwa lugha ya Kiswahili wakati mawasiliano mengine yote yanafanyika kwa kiingereza.
Prof. Lumumba amewataka waandaaji wa makongamano haya kuyaandaa kwa lugha ya Kiswahili kwa kuwa hamna jamii inayopata maendeleo endelevu duniani kwa kutumia lugha za watu wengine na kutokana na umuhimu wa kinachojadiliwa katika kongamano hilo, hamna haja ya kongamano hilo kufanyika kwa Kiingereza.
Prof. Lumumba amewataka wataalamu, wadau na wasomi kutafsiri masuala yote ya uhifadhi kwa lugha nyepesi inayoeleweka kiurahisi ili wananchi waweze kuelewa kinachozungumzwa kwa lugha rahisi ili waweze kufanya mabadiliko yanayohitajika katika kuitunza bioanuai ya bonde la Mto Mara.
Aidha, Prof. Lumumba amezitaka Serikali za Kenya na Tanzania kwa kutumia mapato yake ya ndani kufadhili shughuli zote za maadhimisho ya Siku ya Mara kuonyesha umuhimu wake na kuacha kutumia ufadhili wa mashirika ya kimataifa kufadhili suala muhimu kama maadhimisho ya Siku ya Mara.
Prof. Lumumba amesema kuna manufaa makubwa sana katika uhifadhi wa ikolojia ya Bonde la Mto Mara kwa wananchi wa maeneo hayo, watu walioajiriwa katika hifadhi hizo na Serikali za Kenya na Tanzania kutokana na idadi kubwa ya watalii wanaotembelea hifadhi za Masai Mara na Serengeti.
Prof. Lumumba amesema Serikali zinapata fedha nyingi kutokana na ikolojia iliyopo sasa ya Masai Mara na Serengeti inayoruhusu wanyama kuendelea kuzaliana na kuishi katika hifadhi hizo na kuwavutia watalii wengi kuzitembelea hifadhi hizo hata hivyo zinaruhusu shughuli za viwanda, kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu kwenye bonde la Mto Mara.
Akihitimisha hotuba yake kwenye kongamano hilo, Prof. Lumumba amewaomba waandaaji kuhakikisha kuwa kwenye kongamano lijalo wanasayansi wanawaleta wananchi wanaoishi kwenye Bonde la Mto Mara kutoa ushuhuda wa manufaa waliyoyapata baada ya wanasayansi hao kufanyanao kazi yenye manufaa katika uhifadhi wa ikolojia ya bonde la Mto Mara.
Kongamano hilo limewahusisha maafisa kutoka Serikali ya Tanzania, Kenya na Uganda, wanasayansi kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali, wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Masai Mara na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yaliyofadhili kongamano hilo.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) Dkt. Masinde Bwire amesema kongamano hilo limefanyika wakati muafaka wakati kuna changamoto mbalimbali katika uhifadhi wa Bonde la Mto Mara.
Dkt. Bwire amesema kongamano hilo limekuja wakati kuna mahitaji makubwa ya uhifadhi wa ikolojia ya bonde la Mto Mara kwa ajili ya kuzilinda Hifadhi za Serengeti iliyopo Tanzania na Masai Mara iliyopo nchini Kenya.
Dkt. Bwire amewashukuru washiriki wote walioshiriki kongamano hilo na kuwataka washiriki kushiriki kikamilifu katika kutoa mawazo, maoni na ushauri ambao utasaidia katika kutoa elimu mpya, kubadilisha sera na kuwasaidia wananchi kulinda ikolojia ya bonde la Mto Mara.
Kongamano la pili la kisayansi kuhusu ikolojia ya Mto Mara ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mara yaliyoanza tarehe 13 Septemba, 2024 na kilele chake kinatarajiwa kuwa kesho tarehe 15 Septemba, 2024 katika Mji wa Sekanani, Narok nchini Kenya.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa