Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amezungumza na waandishi wa habari kuhusiana na zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 10 Septemba, 2024.
Mhe. Mtambi amemewapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao na walliokuwa wanajiandikisha kwa mara ya kwanza katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pamoja na wadau mbalimbali waliosaidia kufanikisha zoezi hilo kwa ufanisi.
“Mpaka sasa kwa namna wananchi walivyojitokeza tumevuka lengo mara dufu na katika baadhi ya vituo tumehitajika kuongeza mashine na watumishi ili kuwahudumia watu waliojitokeza kwa wakati” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema watu waliojiandikisha kwa mara ya kwanza ikiwemo vijana na watu wazima ni wengi sana na kuufanya Mkoa kuvuka maradufu lengo lake la awali la uandikishaji na uboreshaji wa taarifa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kanali Mtambi amesema zoezi hilo limefanyika kwa uwazi, utulivu na maelewano ya hali ya juu baina ya Serikali, Vyama vya siasa na wadau mbalimbali wa uchaguzi na kuchukua fursa hiyo kuwashukuru kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika kipindi chote cha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi amesema wakati wa uboreshaji hakukuwepo wimbi la wageni kutaka kujiandikisha baada ya Mkoa wa Mara kuchukua tahadhari za mapema za kudhibiti watu wasiotambulika kujiandikisha kwa kutoa elimu kwa wadau wote ili kusaidiana katika kuwabaini watu wanaopaswa kuboresha taarifa zao.
Kwa upande wake, Mratibu wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Uchaguzi Mkoa wa Mara Bwana Dominicus Lusasi amesema mwitikio wa wananchi katika vituo vya kuboreshea taarifa na hususan katika maeneo ya pembezoni mwa miji ambapo kuna makazi mapya ni mkubwa sana na kulazimisha kuongezwa kwa vituo, mashine na watumishi ili kuwahudumia wananchi.
Bwana Lusasi amesema kutokana na udhibiti uliofanyika katika maeneo ya mpaka, Mkoa umeandikisha Watanzania waliokuwa na sifa za kuandikishwa na kuvipongeza vyama vya siasa kwa kusimamia kwa ukaribu na kutoa mrejesho kwa wakati wanapobaini kasoro yoyote katika zoezi hilo.
Bwana Lusasi ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kuratibu vizuri zoezi hilo jambo ambalo limeurahisishia Mkoa katika usimamizi wa zoezi kwa kiasi kikubwa na kuwashukuru wasimamizi wa zoezi la uboreshaji katika majimbo na kata ambao wamesimamia zoezi hilo kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Bi. Dotto Kulwa Paulo mwanafunzi wa Kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Bweri amesema yeye amejiandikisha kwa mara ya kwanza kwa kuwa ana umri wa miaka 18 kwa sasa na anategemea atakitumia kitambulisho hicho kwa ajili ya kupiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Bi. Dotto amesema watu wengi wamejitokeza katika kituo cha Shule ya Sekondari Bweri muda mwingi wa uandikishaji na leo watu ni wengi zaidi kwa kuwa wanaelewa kuwa leo ndio mwisho wa zoezi hili kwa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa