Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo tarehe 5 Septemba, 2024 amefanya mkutano na wananchi wa Kijiji cha Mikomaliro katika Wilaya ya Bunda kusikiliza kero zao na kuamuru Bwana Magambo Makori mwenye shamba katika eneo linalogombaniwa aondoke katika eneo hilo.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya Mkuu wa Mkoa kusikiliza hoja za wananchi wa eneo hilo akiwa ameambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Bunda pamoja na Maafisa kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Mara.
“Ninaelekeza Mkuu wa Wilaya ya Bunda na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara kusimamia zoezi la kuhakikisha Bwana Magambo anahama katika eneo hilo ili kumaliza mgogod na wananchi hawa” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, Mhe. Mtambi amemtaka Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara kuwakamata watu wanaosadikiwa kuwa sio raia wa Tanzania waliopo katika shamba la Bwana Magambo mara moja ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi kuendelea na shughuli zao katika eneo hilo na wakati Serikali ikiendelea kuangalia suluhisho la kudumu katika eneo hilo lenye mgogoro kati ya kijiji hicho na Kijiji cha Rwemgolori cha Wilaya ya Serengeti.
Kanali Mtambi amesema amekataa mapendekezo ya wataalamu kuwa eneo hilo lenye migogoro lichukuliwe na ianzishwe taasisi ya Serikali au lipewe jeshi kwa kuwa ameona wananchi wanalihitaji ndio maana wanaligombania.
Aidha, amewataka wananchi hao kuacha kutumia nguvu kubwa na ubabe katika eneo hili wakati suluhu ya kudumu ya mgogoro huo ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao za maendeleo.
Awali, wananchi wa eneo hilo wameanzisha mgogoro na kugomea kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wakiishinikiza Serikali kumuondoa Bwana Magambo Magori ambaye wanadai amevamia eneo lao lililotengwa na kijiji cha ajili ya malisho ya mifugo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa