Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amezungumza na machifu na viongozi wa kimila wa Mkoa wa Mara na kuwataka machifu kuisaidia Tanzania kwa kuielimisha jamii na hususan vijana kuhusiana na uzalendo kwa Taifa na mambo mbalimbali ambayo Serikali imeyafanya ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amesema machifu na viongozi wa kimila wachukue nafasi yao katika jamii katika kuwaelimisha vijana wasipotoshwe na taarifa za uongo na wakaichezea amani na utulivu uliopo hapa nchini kwa sasa.
“Ninatamani kuona machifu na viongozi wa kimila mkichukua nafasi yenu katika jamii kwa kuielimisha na kuiongoza jamii katika njia njema yenye kuleta maendeleo endelevu , amani na utulivu wa nchi yetu”amesema Mhe. Mtambi.
Amewataka Machifu na viongozi wa kimila kuacha kuiachia mitandao ya kijamii na wapotoshaji wachache waiharibu nchi yetu na badala yake amewataka viongozi hao kuchukua nafasi zao katika jamii na kuzitumia kuisaidia Serikali katika kujenga amani na mshikamano katika jamii.
Mhe. Mtambi amewatahadharisha viongozi hao kuwa Tanzania ikiwa haina amani wao kama wazee watapata mazingira magumu zaidi kwa kuwa watatamani amani na mshikamano uliopo urudi ili waendelee kama zamani na hawataweza kujiokoa kwa kukimbia kutokana na nguvu za mwili kupungua kutokana na umri wao.
Mhe. Mtambi amewataka machifu na viongozi wa kimila kuihamasisha jamii kuwakataa waganga feki wenye ramli chonganishi na wanaowadanganya watu kuhusu kupata utajiri wa haraka na wakati mwingine wakitaka wawadhuru watu wengine ili wao wapate utajiri.
Mkuu wa Mkoa wa Mara ameagiza maeneo yote yaliyokuwa yanatumika na viongozi wa kimila na machifu kwa ajili ya vikao na matambiko yalindwe na waliyoyavamia waondoke ili machifu na viongozi wa kimila wapate maeneo ya kufanyia shughuli zao.
Aidha, amewataka viongozi wa Serikali Mkoa wa Mara kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutoa ushirikiano kwa machifu na viongozi wa kimila waliopo kwenye maeneo yao na kuwashirikisha katika shughuli za Serikali.
Mhe. Mtambi pia ametumia kikao hicho na kutoa ufafanuzi kuhusu eneo la ardhi ya Manispaa ya Musoma na kuwaeleza kuwa udogo wa eneo ukichukuliwa vizuri inaweza kuwa fursa ya kuleta maendeleo kwa wananchi na hususan wakielimishwa vizuri namna ya kulitumia eneo hilo.
Kanali Mtambi amesema mpango wa serikali kwa sasa sio kuongeza eneo katika Manispaa ya Musoma bali ni kuanza kujenga magorofa na h`ususan majengo ya Serikali ili kulitumia vizuri eneo lililopo kwa maendeleo ya wananchi wa Musoma.
Akizungumza na machifu na viongozi wa kimila hao, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama cha Mapunduzi Mhe. Maganya Fadhili Rajabu ameshukuru sana kwa kukaribishwa katika kikao hicho na kuwataka viongozi hao kukisemea vizuri Chama cha Mapinduzi katika jamii.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. Samia Suluhu Hassan anawatambua na kuwathamini machifu na viongozi wa kimila kutokana na umuhimu wenu katika jamii, ninawaomba mtumie nafasi mliyonayo kuisaidia Serikali” amesema Mhe. Rajabu
Mhe. Rajabu amesema kwa vijana wanaweza wasielewe nchi ilikotoka hadi kufika hatua hii iliyopo sasa na kwamba kuna kazi kubwa ambayo Serikali imeifanya tangia nchi ilipopata uhuru mpaka wakati huu ambapo kuna maendeleo makubwa yamefanyika.
Mhe. Rajabu amewataka viongozi hao kukemea mauaji ya watu, mapenzi ya jinsia moja, mmomonyoko wa maadili na kusimamia malezi na maadili ya vijana ili waachana na tabia za kuiga mambo ya kwenye mitandao bila ya kuyafikiria kiundani kuhusu uzuri na ubaya wake katika jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Machifu wa Mkoa wa Mara, Chifu Deus Masanja amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kumpatina nafasi kuzungumza na viongozi hao na kuzungumzia umuhimu wa vijana kupewa elimu kuhusu uzalendo na utaifa wao.
wa kimila wa Mkoa wa Mara na kutenga muda wa kuzungumza nao.
Chifu Masanja amesema tatizo la waganga feki na chonganishi katika jamii linatokana na mfumo mpya wa utoaji wa vibali zamani vibali hivyo vilikuwa vinatolewa na machifu na viongozi wa kimila baada ya kuwapima waganga hao na kujua mwelekeo wao na kama kweli ni waganga.
“Sasa hivi vibali vya waganga wa kienyeji kufanya kazi katika jamii vinatolewa na maafisa wa Serikali ambao hawana uwezo wa kutambua kama wanayempatia kibali ni mganga au ni mganga feki, mwizi na wachonganishi katika jamii”amesema Chifu Masanja.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji kulihudhuriwa na machifu na viongozi wa kimila 17 kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Mara, viongozi wa Jumuiya ya Wazazi na Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara na baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa