Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao cha maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 na Maonyesho ya Sikukuu ya Wakulima (NANENANE) kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji na kuzungumzia mpango wake wa kuanzisha tuzo maalum kwa Halmashauri na Wilaya zitakazofanya vizuri kwenye Mbio za Mwenge wa Uhuru kuanzia mwaka 2024.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amesema Mkoa utatoa tuzo kwa Halmashauri mbili zitakazoongoza na Halmashauri mbili zitakazokuwa za mwisho katika matokeo ya mbio za Mwenge wa Uhuru yatakayotangazwa kitaifa.
“Tunzo ya washindi itakuwa cheti na kombe wakati tunzo ya waliofanya vibaya itakuwa ni kinyago kinachowazomea ambacho kitawekwa kwenye ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Wilaya ambao Halmashauri zao zimefaya vibaya” amesema Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema kuwa gharama za kutengeneza tuzo hizo zitatolewa na Halmashauri zilizofanya vibaya baada ya Mkoa kumtafuta mzabuni wa kutengeneza tuzo hizo na kuzitaka Halmashauri kuzingatia miongozo na maelekezo yote ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024.
Kanali Mtambi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kuwa maandalizi ya shughuli za Mwenge wa Uhuru zinazingatia mwongozo na maelekezo ya kitaifa na kuondoka kasoro zilizojitokeza katika mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka jana.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara amefuta likizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Wilaya ili waweze kusimamia kikamilifu maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru na maandalizi ya maonyesho ya NANENANE kwa mwaka 2024.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara amezitaka Halmashauri kujiandaa mapema kufanikisha shughuli za mbio za Mwenge wa Uhuru na NANENANE ambazo zitafanyika kwa wakati mmoja na kuhitaji umakini zaidi katika maandalizi yake.
Bwana Kusaya ameeleza kuwa Halmashauri zitapewa kiasi kinachohitajika katika michango ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 baada ya Wakuu wa Mikoa kuamua kuhusiana na mapendekezo ya michango hiyo.
Katibu Tawala amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kulipa mapema fedha za maandalizi ya matukio haya kwa kuzingatia usumbufu wa mifumo ya malipo wakati ambapo malipo hayo yatakapokuwa yanahitajika.
Aidha, Bwana Kusaya amewataka Wakurugenzi kusimamia mashamba yao waliyopewa katika Shamba la Mkoa wa Mara lililopo Wilaya ya Butiama ili wakulima wa Mkoa wa Mara waweze kupewa elimu katika shamba hilo.
Awali, akitoa taarifa katika kikao hicho, Mratibu wa Mwenge Mkoa wa Mara Bwana Fidel Baragaye ameeleza kuwa katika mbio za mwaka jana miradi yote 63 iliyopangwa na Mkoa ilipitishwa na Mwenge wa Uhuru.
Bwana Baragaye ameyataja mafanikio mengine kuwa ni Mkoa wa Mara ulishika nafasi ya 8 kitaifa kati ya mikoa 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyokimbiza Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 ambapo ulipanda ukilinganisha na nafasi ya 12 kwa mwaka 2022.
Bwana Baragaye amezitaja Halmashauri zilizofanya vizuri kuwa ni pamoja na Halmashauri ya Mji wa Tarime, Halmashauri ya Mji wa Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda; wakati Halmashauri ambayo haikufanya vizuri katika mbio hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Bwana Baragaye ameeleza kuwa kwa mwaka huu, Mwenge unategemewa kupokelewa tarehe 26 Julai, 2024 katika Wilaya ya Serengeti na kukimbizwa katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara kabla ya kukabidhiwa katika Mkoa wa Simiyu tarehe 4 Agosti, 2024.
Akizungumzia kuhusu mikakati ya mwaka huu, Bwana Baragaye ameeleza kuwa Mkoa umejipanga kuboresha zaidi kwa kukagua kikamilifu maelekezo yote hususan katika maandalizi na uwasilishaji wa risala za utii, uzingatiaji wa vigezo vya Mwenge wa Uhuru na kupunguza au kuondoa kabisa baadhi ya changamoto wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mhandisi Mwita Okayo ameeleza kuwa Halmashauri zinapaswa kujipanga kutekeleza mwongozo wa kitaifa wa maonyesho ya NANENANE ikiwa ni pamoja na kupanga bajeti mapema na kuweka vipando katika eneo la maonyesho.
Mhandisi Okayo ameeleza kuwa Mkoa wa Mara unategemea kushiriki maonyesho ya NANENANE katika viwanja vya Nyakabindi, Mkoa wa Simiyu ambapo mikoa yote ya Kanda ya Ziwa Mashariki itashiriki maonyesho hayo katika viwanja hivyo.
Mhandisi Okayo ameitaja Mikoa itakayohusika kuwa ni pamoja na Mkoa wa Mara, Simiyu na Shinyanga na kuzikumbusha Halmashauri kulipia ada ya ushiriki mapema iwezekanavyo na ameikishukuru Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu kwa kuziwezesha Halmashauri za Mkoa wa Mara mbolea ya kupandia na kukuzia bure.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, maafisa kilimo na waratibu wa shughuli za Mwenge wa Uhuru na NANENANE katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa