Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi tarehe 25 Aprili, 2024 amefunga mafunzo ya Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kuwataka watumishi hao kuwasikiliza, kushughulikia na kutatua kero za wananchi katika maeneo yao.
“Wasikilizeni wananchi na kuchukua hatua stahiki kutatua kero hizo na kama kuna jambo hulielewi uliza wenzio na viongozi wa juu zaidi na kama linakushinda mwelimishe mwananchi kwenda ngazi inayofuata” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka Watendaji wa Kata kuwasaidia wananchi kwa kutambua mahitaji na mategemeo halisi ya wananchi na kuyaingiza katika Mpango wa Maendeleo ya Kata na baadaye uingizwe katika Mpango wa Maendeleo ya Halmashauri.
Kanali Mtambi amewataka maafisa hao kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao kwa weredi kwani Serikali inapeleka fedha nyingi katika Tarafa na Kata hapa nchini ili kuboresha huduma za jamii kwa wananchi wake.
“Mhakikishe kuwa fedha zilizotolewa zinatumika kufanyakazi iliyokusudiwa, kusimamia uchaguzi wa maeneo ya kujenga miradi na thamani halisi ya miradi hiyo ili kutoa taarifa kwa wananchi “ amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, amewataka kusimamia utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti, kusimamia mpango wa matumizi sahihi ya ardhi, kupambana kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii, kukemea vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kukemea kilimo cha bangi katika maeneo yao.
Kanali Mtambi amewataka kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 na hususan katika zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura litakalofanyika hivi karibuni.
Mhe. Mtambi amewataka kuanza maandalizi yam bio za Mwenge wa Uhuru katika maeneo yao ambapo Mkoa wa Mara utapokea Mwenge wa Uhuru tarehe 26 Julai, 2024 hadi tarehe 3 Agosti, 2024 utakapoukabidhi Mkoa wa Simiyu kuendelea na mbio zake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI Bwana Ibrahim Minja amesema jumla ya Maafisa Tarafa 300 na Watendaji wa Kata 2,260 wamepatiwa mafunzo katika mikoa 16 ya Tanzania Bara tangu mafunzo hayo yalipoanza kutolewa.
Bwana Minja amesema lengo la TAMISEMI ni kutoa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wa Mikoa yote kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 kwa kuwa hawa ndio viongozi wanaotekeleza majukumu yao karibu na wananchi.
Mafunzo haya yalifunguliwa tarehe 24 Aprili, 2024 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya na kuendeshwa na wataalamu kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na Chuo cha Utumishi wa Umma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa