Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amezungumza na viongozi na watendaji wa Halmashauri za Mkoa wa Mara kuhusiana na utoaji wa chakula shuleni na kuagiza shule zote za msingi na sekondari zijenge jiko na stoo ifikapo tarehe 31 Desemba, 2024.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo baada ya Shirika la Pamoja Tuwalishe kuahidi kutoa majiko banifu na masufuria na misaada mingine kwa shule ambazo zitahamasisha wazazi na walezi kuchangia ujenzi wa majiko na stoo kwa mujibu wa ramani iliyotolewa na shirika hilo.
“Hii ni fursa kubwa Mkoa wa Mara tumeipata, ni lazima viongozi tuhakikishe wananchi wetu wanaichangamkia ili kujenga miundombinu itakayowezesha utoaji wa chakula shuleni” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya kutoa taarifa ofisini kwake kuhusiana na maandalizi ya ujenzi wa majiko hayo na utoaji wa chakula shuleni kila mwisho wa mwezi ili kuuwezeha Mkoa kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhusiana na suala hilo.
Mhe. Mtambi amewaagiza Wakuu wa Wilaya kuongeza kipengele cha hali ya utoaji wa chakula shuleni katika taarifa za Wilaya kila anapofanya ziara katika Wilaya hizo ili kupata hali halisi iliyopo, mikakati ya Wilaya katika utoaji wa chakula shuleni na changamoto kama zipo.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Pamoja Tuwalishe kwa Mikoa ya Dodoma na Mara Bwana Godfrey Paul Machumu ameeleza kuwa ili kutoa chakula shuleni kwa ufanisi, Shirika hilo limebuni majiko sanifu na stoo kwa ajili ya kuhifadhia na kupikia chakula cha wananfunzi.
Hata hivyo, masharti ya kupewa majiko hayo ni shule kuwahamasisha wazazi na walezi kuchangia ili shirika liweze kuwafungia majuko hayo pamoja na masufuria ya kupikia chakula cha wanafunzi.
“Kwa sasa Shirika linazo bati 400 za kuezekea maboma hayo ambazo litazitoa kama motisha kwa shule zitakazoweka kukamilisha ujenzi wa maboma mapema katika Mkoa wa Mara”. amesema Bwana Machumu na kuongeza kuwa
Bwana Machumu amesema Shirika hilo pia linatoa mchoro na makadirio ya ujenzi (BoQ) kwa shule zote ili shule ziweze kujenga majengo hayo kwa ubora na viwango vinavyohitajika na baada ya majengo hayo kukamilika, Shirika litawajengea mfumo wa unawaji kwa ajili ya wanafunzi ili kuhakikisha chakula kinaliwa katika mazingira salama.
Bwana Machumu amesema kuwa Shirika hilo pia linatoa mafunzo, mbegu na mfumo wa umwagiliaji kwa shule ambazo zina maeneo kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula, matunda na mbogamboga ili kuboresha utoaji wa chakula shuleni.
“Shirika linatoa pia vishikwambi kwa ajili ya ujazaji wa taarifa za chakula shuleni na kwa ajili ya viongozi kufuatilia utoaji wa chakula shuleni ili kuwawezesha viongozi kutambua wanafunzi ambao wamekula kila siku kupitia mfumo maalum wa ufuatiliaji” amesema Bwana Machumu.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na Halmashauri za Wilaya na Shirika la Pamoja Tuwalishe.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bi. Judith Mrimi amesema kwa sasa utoaji wa chakula shuleni katika Mkoa wa Mara hauridhishi na takwimu zinaonyesha hadi kufikia Septemba, 2024 ni asilimia 56 tu ya wanafunzi wa shule za msingi na asilimia 59 ya wanafunzi wa shule za Sekondari ndio wanapata chakula shuleni.
“Chakula kikuu kinacholiwa katika shule nyingi ni uji na makande kwa mwaka mmzima na shule nyingi zinatoa chakula katika msimu wa mavuno tu au katika madarasa ya mitihani na katika vipindi vya mitihani” amesema Bibi. Mrimi.
Hata hivyo Bibi Mrimi ameelezea utafiti uliofanywa na Shirika la Twaweza mwaka 2019 ulioonyesha kuwa asimilia 100 ya wanafunzi wanaosoma Haknashauri ya Wilaya ya Moshi (Kilimanjaro), asilimia 96.6 Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa (Njombe) na asilimia 93.3 ya Wilaya ya Rombo (Kilimanjaro) walikuwa wanakula shuleni.
Bibi Mrimi ametoa wito kwa viongozi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Shirika la Global Communities katika ujenzi wa miundombinu ya jiko na stoo ya chakula shuleni ili kuwawezesha asilimia 100 ya wanafunzi wote kupata angalau mlo mmoja wakiwa shuleni.
Kwa upande wake, Bwana Godfrey Paul Machumu, Meneja wa Mradi wa Pamoja Tuwalishe kwa Mikoa ya Mara na Dodoma amesema Shirika la Project Concern International (PCI) limekuwa likifayakazi katika mkoa wa Mara katika miaka ya 2011-2021 kabla ya kuja tena kama Pamoja Tuwalishe.
Bwana Machumu amesema awali shirika hilo lilikuwa linatoa msaada wa chakula shuleni kwa shule 247 za Mkoa wa Mara katika Wilaya za Musoma, Butiama na Bunda na kwa sasa linatoa msaada wa chakula katika shule 45 za Rorya, Tarime na Serengeti.
Bwana Machumu amesema tofauti na awali, utoaji wa chakula wa sasa unachangiwa na wazazi pia ambapo kuna siku shirika linatoa chakula na kuna siku za wazazi pia kutoa chakula na hadi kufikia mwaka wa tano wa mradi, wazazi watatoa chakula kwa siku zote.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa