Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amewaongoza wananchi katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya Elimu ya Watu Wazima, Elimu Maalum na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi yaliyofanyika katika uwanja wa Right to Play, Wilaya ya Serengeti na kuzitaka Halmashauri kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya Elimu ya Watu Wazima.
“Mimi nitafuatilia kuhakikisha Halmashauri zote zinatenga bajeti inayotosheleza shughuli za Elimu ya Watu Wazima ili kutekeleza majukumu ya Halmashauri katika Elimu ya Watu Wazima kwa ufanisi” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao wanaenda shule na wanasoma kwa bidi na kutoa onyo kwa wazazi ambao wanagoma kuchangia chakula cha watoto shuleni na kuwatahadharisha kuwa Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria wazazi wote ambao hawachangii chakula cha wanafunzi shuleni.
Kanali Mtambi amewataka wazazi na walezi kujidhatiti katika kulea watoto wao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanapata chakula cha mchana wakiwa shuleni ili waweze kujifunza vizuri na kuacha kuwafanyia ukatili wa kuwashindisha njaa wanafunzi muda wote wanapokuwa shuleni.
Mhe. Mtambi ametumia muda huo pia kuzungumza na wanafunzi na kuwataka kuzingatia masomo na kusoma kwa bidi na kuacha mara moja kufanya tabia mbaya za utoro na utovu wa nidhamu na mambo yasiyofaa wakiwa shuleni.
Mhe. Mtambi amesema elimu ya watu wazima ni jitihada za Serikali za kuhakikisha watu wote wanapata elimu bila kujali sehemu walipo, hali zao na uchumi wao na amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kujiendeleza na kujifunza ujuzi mpya kila wakati ili waweze kuboresha maisha yao na familia zao.
Mhe. Mtambi amewapongeza wananchi wa Wilaya ya Serengeti kwa kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo na kuwataka kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika hapa nchini tarehe 27 Novemba, 2024.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo Bwana Makwasa Bulenga amesema maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi yanalengo la kuomarisha utaratibu, usimamizi na kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa shughuli za elimu.
Bwana Bulenga amesema mataifa mbalimbali duniani wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, Utamaduni (UNESCO) huungana katika kupima na kutafakari mafanikio na changamoto zilizopo katika utoaji wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi yenye adhma ya kufuta ujinga, umaskini na maradhi.
Bwana Bulenga amesema maadhimisho haya hufayika kila mwaka tarehe 1-8 Septemba katika Mikoa na Halmashauri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Ujumuishi katika Elimu bila ukomo kwa Ujuzi, Ustahimilivu, Amani na Maendeleo”
Bwana Bulenga amesema katika Mkoa wa Mara, Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA) una wanafunzi 2,463 ambapo wavulana ni 1,292 na wasichana ni 1,171 wanaosoma katika shule na vituo 127.
Bwana Bulenga amesema Mpango wa Uwiano kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA) ambao unawahusisha watu wazima kuanzia miaka 18 na kuendelea unatekelezwa katika vituo 69 yenye wanakisomo 1,357 ambapo huhudisha shughuli za ujasiriamali, kilimo, ufugaji, kilimo pamoja na kujifunza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wasiojua stadi hizo.
Bwana Bulenga amesema kuwa Mkoa wa Mara una vituo nane katika Halmashauri nane vyenye wanafunzi wakike 190 waliorudi shule baada ya kukatiza masomo katika mfumo rasmi kutokana na sababu mbalimbali.
Bwana Bulenga ameyataja mafanikio kuwa ni pamoja na wanafunzi wa MEMKWA 399 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na wanafunzi 310 walifaulu na kuendelea na masomo ya sekondari na kati ya wasichana 59 waliofanya mtihani wa kidato cha nne, wasichana 16 walifaulu na kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita.
Katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa ametembelea mabanda ya maonyesho ya shughuli mbalimbali za elimu na kutoa zawadi kwa wanafunzi, walimu na shule zilizofanya vizuri katika maeneo mbalimbali.
Maadhimisho ya wiki ya Elimu ya Watu Wazima yamehudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti, Maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, viongozi na watendaji wa Halmashauri, wanachi na wanafunzi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa