Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao cha kujadili maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na kuzipongeza Halmashauri zilizopata hati safi katika ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amesema Halmashauri nane za Mkoa wa Mara zimepata hati safi wakati Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ikiwa imepata hati isiyoridhisha katika ukaguzi wa CAG kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
“Ninawapongeza sana kwa kazi kubwa iliyofanywa na Halmashauri za Mkoa wa Mara katika kufunga hesabu za Serikali na kutoa ufafanuzi unaohitajika kwa wakaguzi wa hesabu za serikali” amesema Kanali Mtambi na kuitaka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuchukua hatua kurekebisha hati hiyo katika kaguzi zijazo.
Mhe. Mtambi ameelekeza Kamati za Fedha na Mipango za Halmashauri kuwachukulia hatua watumishi ambao kwa namna moja au nyingine walisababisha hoja za ukaguzi kutokana na uzembe na ofisi yake ipate taarifa ya hatua zilizochukuliwa kwa watumishi hao.
Mhe. Mtambi amezitaka Halmashauri kuyafanyia kazi maagizo yote ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) na hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na hoja za miaka ya nyuma.
Aidha, ameyataka Mabaraza ya Madiwani katika Halmashauri kusimamia matumizi ya fedha za wajibu wa migodi kwa jamii (CSR) ili miradi inayotekelezwa kwa fedha za CSR iweze kukamilika kwa wakati kwa kutumia bajeti iliyopangwa.
Kanali Mtambi amezitaka Halmashauri kuendelea na maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru ambapo Mkoa wa Mara unategemea kupokea Mwenge wa Uhuru tarehe 26 Julai, 2024 hadi tarehe 3 Julai, 2024 na kuzitaka Halmashauri kutoa kipaumbele katika maandalizi ya mapokezi na Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024.
Mtambi amezitaka Halmashauri kuacha kutumia fedha za makusanyo kabla ya kupelekwa Benki na kuzitaka kufuata miongozo, sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya fedha za Serikali na kufanya usuluhishi wa mahesabu kabla ya tarehe 10 ya kila mwezi.
Mhe. Mtambi amewataka viongozi na watendaji wa Halmashauri kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao na kuratibu kero zilizotatuliwa katika kila ngazi ili kupata rejea inapoibuka tena sehemu nyingine.
Kwa upande wake, akitoa taarifa katika kikao hicho Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Menejimenti ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi (MMI) Bwana Marco Maduhu ameeleza kuwa LAAC iliziita Halmashauri sita za Mkoa wa Mara kwenda Dodoma na kuzitembelea Halmashauri tatu ambazo hazikuitwa Dodoma na kutoa maagizo mbalimbali.
Bwana Maduhu ameeleza kuwa LAAC ilitoa jumla ya maagizo 45 kwa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara na kati ya hayo maagizo manne yamejibiwa, maagizo 21 yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na maagizo 20 hayajatekelezwa.
Kikao hicho kimehudhuriwa na waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Menejimenti ya Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya, Kamati za Fedha za Halmashauri na Menejimenti zote za Halmashauri za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa