Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo tarehe 5 Septemba, 2024 amezingua zoezi la utoaji wa fidia kwa wananchi wa Kata ya Nyatwali, Wilaya ya Bunda wanaohama kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA).
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Mtambi amesema Serikali imeruhusu wananchi hao kupata nyongeza ya fidia yao kwa asilimia 7 baada ya malipo hayo kuchelewa baada ya tathmini ya eneo hilo kukamilika kutokana na sababu mbalimbali na kuwahamasisha kuondoka mapema baada ya kupata malipo yao.
“Ni vizuri mkipata pesa ya fidia kabla hamjaanza kufanya mambo mengine muondoke mapema katika eneo hili kabla ya fedha mnazopata hamjatumia kwenye mambo mengine yasiyo na msingi” amesema Mhe. Mtambi.
Amewataka viongozi wa eneo hilo kuonyesha mfano kwa kuanza kuondoka mapema na kuzitaka familia kujadili kwa undani namna ya kwenda kujenga familia zao katika maeneo mengine watakayoamua kwenda kuanzisha maisha yao.
Mhe. Mtambi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele cha malipo ya fidia kwa wananchi wa Kata ya Nyatwali na kuwawezesha wananchi hao kwenda kuishi maisha yao katika mazingira salama mbali na wanyama wanaotoka katika hifadhi.
“Hili ni eneo la mapito ya asili ya wanyama na ambalo lina manufaa makubwa katika ikolojia na fursa mbalimbali za utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Ziwa Victoria” amesema Mhe. Mtambi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini Mhe. Robert Maboto ameipongeza Serikali kwa kukamilisha mchakato wa malipo na kuiomba Serikali kutoa elimu ya kutosha ya namna zoezi la ulipaji wa fidia litakavyofanyika.
“Wananchi hawa wapo tayari kusikiliza maelekezo ya Serikali kuhusiana na zoezi hili tuwaeleweshe vizuri wananchi ili kuondoa malalamiko ya wananchi hapo baadaye” Mhe. Maboto.
Kwa upande wake, mwananchi wa Mtaa wa Kariakoo katika Kata ya Nyatwali amesema Bibi Mgesi Kisuka Machira ameishukuru Serikali kwa kutoa malipo hayo waliyokuwa wanayasubiri kwa muda mrefu na kuahidi atahama eneo hilo mapema iwezekanavyo.
“Tunamshukuru Rais kwa kutoa malipo ya kuhamishwa, kero za wanyama waharibifu tutaondokana nazo ikiwemo kuvamiwa na mamba, kiboko, tembo na wanyama wengine mara kwa mara” amesema Machira.
Bibi Machira ambaye ndiye amekabidhiwa Washima amesema amefurahia kwa kuwa Serikali imewaruhusu kwenda na vitu vyote walivyokuwa navyo ikiwemo matofali, mabati na miti ambavyo watavitumia huko wanakoenda.
Zaidi ya wananchi 3,500 wa Kata ya Nyatwali wanategemea kulipwa fidia na Seriklai kupitia Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ambapo jumla ya shilingi 45.9 kimetengwa kwa ajili ya malipo ya wananchi kutokana na eneo hilo kupitiwa na wanyamapori kutoka SENAPA wakati wa kiangazi wanapokwenda kunywa maji Ziwa Victoria katika ghuba ya Speke.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa