Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 12 Juni, 2025 amezindua kongamano la wamawake wa Kanisa la Tanzania Missionary Revival Church (TMRC) katika eneo la Kigera, Manispaa ya Musoma na kuwataka wanawake kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kuwania nafasi za uongozi.
Mhe. Mtambi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha mfano kuwa viongozi wanawake wanatekeleza vizuri majukumu yake na kuwataka wanawake zaidi kugombea nafasi za ubunge, udiwani katika nafasi hiyo.
“Kwa sasa Mama amewasafishia njia hata ambao walikuwa hawaamini kwa mfano huu Mhe. Rais alioutoa hapa nchini kwa sasa kila mtu anaamini wanawake wanaweza na wanafanya vizuri kuliko wanaume” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema wanawake waliopewa nafasi mbalimbali za uwaziri, ubunge na udiwani wanafanya vizuri na kuongeza kuwa hapo baadae inaweza kuwa vigumu kwa wanaume kugombea kwa kuwa wanawake waliopewa nafasi mbalimbali wanafanya vizuri sana.
Mhe. Mtambi amewataka kuliombea Taifa na hususan wakati huo nchi inapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kuwahamasisha watu wote kushiriki uchaguzi kwa kupiga kura na kuwachagua viongozi na kama wanasifa kugombea katika uchaguzi huo.
Kanali Mtambi amewataka wanawake hao kuihamasisha jamii kudumisha umoja, amani na mshikamano uliopo bila kubaguana kwa misingi ya dini, siasa na makundi yasiyofaa katika jamii na kuihamasisha jamii kuilinda amani na utulivu uliopo hapa nchini.
Mkuu wa Mkoa amewahakikishia wanawake hao kuwa Serikali inatambua na kuuthamini mchango wa madhehebu ya dini na viongozi wa dini katika maendeleo ya Taifa na kuwataka waumini hao waendelee kuifanya kazi nzuri wanayoifanya katika jamii.
Mhe. Mtambi amewataka kuwahamasisha wazazi na walezi kukemea mmomonyoko wa maadili katika jamii na kulea familia zao kwa misingi ya utamaduni wa Kitanzania ili kupata Taifa bora kwa hapo baadaye na kuwakemea watu wachache katika jamii wanaotumika kwa kudanganywa na wasioitakia mema Tanzania.
Akijibu maombi ya wanawake hao, Kanali Mtambi amewachangia wanawake hao ng’ombe wawili na Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka amechangia ng’ombe mmoja kwa ajili ya chakula kwa siku hizo tano wakiwa katika Manispaa ya Musoma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka amewakaribisha wanawake hao katika Wilaya ya Musoma na kuwashukuru kwa kuchagua kufanyia kongamano hilo katika Wilaya ya Musoma.
Mhe. Chikoka amewapongeza wanawake hao kwa kujitoa kwako kumtumikia Mungu na kuwapongeza kwa kuwa kongamano lao lilikuwa limefana sana.
Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Mara Shekhe Juma Masiroli ambaye pia alishiriki hafla ya ufunguzi wa kongamano hilo amewapongeza wanawake wa TMRC kwa kuamua kufanya kongamano la kuwafundisha masuala mbalimbali muhimu katika jamii.
Sheikh Masiroli amewataka wanawake kuliombea Taifa na hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi, kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuuombea Mkoa wa Mara na wananchi wake amani.
Akisoma risala kwa niaba ya wanawake hao Bi. Leah Jacob Rutabija amesema kongamano hilo linawakutanisha wanawake zaidi ya 400 kutoka mikoa yote hapa nchini na linafanyika kuanzia tarehe 11-15 Juni, 2025 katika eneo la Kigera, Manispaa ya Musoma kwa ajili ya kumuenzi Askofu Mstaafu wa Kanisa hilo Askofu Jacob Rutubija aliyekua kiongozi katika Jimbo la Mara.
Bi. Leah amesema Kongamanao la mwaka huu limeambatana na maombi maalum ya kuliombea Taifa nchi inapoekelea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Bi. Leah alitoa ombi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara kuwasaidia bajeti ya kongamano hilo ambalo litagharimu milioni 20 kwa siku zote tano na kuongeza kuwa tayari akina mama hao wamepata kiasi cha fedha za kuanzia na wanaendelea kuomba michango kutoka kwa wadau mbalimbali.
Hafla ya uzinduzi ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kanisa la TMRC na baadhi ya viongozi na maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa