Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ofisini kwake amezungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 katika Mkoa wa Mara na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili waweze kushiriki uchaguzi huo.
Mhe. Mtambi amesema “kuanzia tarehe 11 hadi 20 Oktoba, 2024 kila mwananchi ajitokeze kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura ili apate haki ya kupiga na kupigiwa kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na mtu asipojiandikisha hataweza kupiga kura katika uchaguzi huo”.
Mhe. Mtambi amesema tarehe 15 Agosti, 2024 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa alitoa tangazo la uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024 na kueleza kuwa utafanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
Mhe. Mtambi amesema katika kuelekeza uchaguzi wa Serikali za Mitaa yapo matukio muhimu ambayo ni pamoja na maelezo kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambayo yatatolewa rasmi tarehe 26 Septemba, 2024 na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo yao ya utawala na uandikishaji wa wapiga kura litakalofanyika kwa siku kumi kuanzia tarehe 11-20 Oktoba, 2024.
Mhe. Mtambi amesema kuwa kila mwananchi anapaswa kujiandikisha katika Kijiji, Mtaa au Kitongoji chake kwenye kituo ambacho atapigia kura, na vituo hivyo vitaainishwa na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo hayo.
Mhe. Mtambi amezitaja sifa za mwananchi anayepaswa kujiandikisha kuwa ni pamoja na awe raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi, awe ni mkazi wa maa, kijiji au kitongoji ambapo uchaguzi unafanyika.
Kanali Mtambi amesema zoezi la kuchukua na kurejesha fomu kwa wanaogombea nafasi za uongozi ni tarehe 01 hadi 07 Novemba, 2024 na zoezi la uteuzi wa wagombea litafanyika tarehe 8 Novemba, 2024 na kuwataka wananchi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali zinazogombaniwa katika uchaguzi huo.
Amezitaja nafasi hizo kuwa ni Mwenyekiti wa Mtaa, wajumbe wa kamati ya mtaa kwa halmashauri za miji na Manispaa; Mwenyekiti wa Kijiji, wenyeviti wa vitongoji na wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji kwa Halmashauri za Wilaya.
Mhe. Mtambi amesema kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa zitafanyika tarehe 20-26 Novemba, 2024 baada ya vyama vya siasa kuwasilisha ratiba ya kampeni zao kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya tarehe 14 Novemba, 2024 kwa mujibu wa mwongozo wa ratiba za uchaguzi.
Kanali Mtambi amevitaka vyama vya siasa kutoa ushirikiano kwa wasimamizi wa uchaguzi na viongozi wa Serikali waliopo katika maeneo yao na kuzingatia ratiba ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 ili uchaguzi ufanyike kwa mujibu wa miongozo, sheria na kanuni.
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na uandikishaji, Mhe. Mtambi amesema katika Mkoa wa Mara kulikuwa na zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura lililofanyika kuanzia tarehe 4 -10 Septemba, 2024, zoezi hilo halihusiani na uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
Kauli mbiu ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024 ni “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi”.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa