Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amezungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kutoa taarifa ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee ambayo kitaifa yatafanyika katika Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara tarehe 15 Juni, 2025.
“Ninaomba kuchukua fursa hii kuwakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa Mara na Mikoa ya jirani kushiriki maadhimisho haya muhimu ambayo kitaifa yatafanyika katika Shule ya Msingi Miembeni, Halmashauri ya Mji wa Bunda” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema mgeni rasmi katika maadhimisho haya atakuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dorothy Gwajima na kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka 2024 ni “Utu, Usalama na Ustawi ni nyenzo ya Kutokomeza Vitendo vya Ukatili dhidi ya Wazee”
Mhe. Mtambi amesema kuwa maadhimisho haya yatatanguliwa na mashindano ya michezo baina ya wazee itakayofanyika tarehe 13 Juni, 2024 katika Chuo cha Ualimu Bunda, kongamano kuhusu masuala mbalimbali ya wazee litakalofanyika Chuo cha Ualimu Bunda na wazee kwenda kutembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwitongo, Butiama tarehe 14 Juni, 2024.
Aidha, kwa siku zote tatu (tarehe 13-15 Juni, 2024) kutakuwepo na upimaji wa afya bure na maonyesho mbalimbali ya shughuli za wazee na kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa tarehe 15 Juni, 2024 katika viwanja vya Shule ya Msingi Miembeni.
Kwa mujibu wa Mhe. Mtambi Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee yameanza kuazimishwa kimataifa mwaka 2011 baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kuzitaka nchi wanachama kuazimisha siku hiyo.
Mhe. Mtambi amesema malengo ya maadhimisho haya ni kutoa elimu, kubadili mitizamo ya jamii kuhusiana na wazee na kuzeeka na kuwasaidia wazee kupata sehemu ya kusemea kero zao zinazowakabili katika jamii.
Mhe. Mtambi amesema Mkoa wa Mara hauna matukio ya kuwanyanyasa wazee na maadhimisho haya yameletwa ili watu wa mikoa mingine wajifunze namna nzuri ya kuishi na kuwatumia wazee kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Mhe. Mtanda amesema maandalizi kwa ajili ya maadhimisho hayo yamekamilika na kuwataka wananchi kujitokeza kupata elimu na kuwapeleka wazee kupima afya zao bure katika muda wote wa siku tatu za maadhimisho hayo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa