Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amefunga maonesho ya tisa ya kilimo mseto yaliyokuwa yanaendelea katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Mseto katika eneo la Bweri, Manispaa ya Musoma na kuwataka wananchi kuendelea kukitumia kituo hicho kujifunza kilimo mseto.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga maonesho hayo, Mhe. Mtambi amesema kuwa kituo hicho ambacho kinamilikiwa na Shirika la Vi Agroforestry ni sehemu muhimu kwa wananchi wa Mkoa wa Mara kwenda kujifunza mambo mbalimbali kuhusu kilimo mseto ili kuweza kubadilisha maisha yao.
“Hapa ni sehemu muhimu sana kwa wananchi kuja kujifunza na kubadilishana mawazo kuhusu kilimo mseto na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu na wazoefu wa kilimo mseto” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amelipongeza shirika la Vi Agroforestry na washirika wake kwa kuandaa maonesho hayo kila mwaka na kukifungua kituo hicho wakati wote ili wananchi waweze kwenda wakati wowote kujifunza kilimo mseto.
Mkuu wa Mkoa amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Mara kuwapeleka wanafunzi kwa nyakati tofauti tofauti wa shule za msingi na sekondari zote za Mkoa wa Mara katika kituo hicho ili eneo hilo liwe linatembelewa wakati wote na watu wanaopenda kujifunza kuhusu kilimo mseto.
Wakati huo huo, Mhe. Mtambi amewataka wananchi waliohudhuria maonesho hayo kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika hapa nchini tarehe 27 Novemba, 2024 hapa nchini na kuongeza kuwa kilimo mseto bila viongozi bora na wapenda maendeleo hamna maendeleo.
Kauli mbiu ya maonesho hayo kwa mwaka huu ni Kilimo Mseto kwa Mifumo Endelevu ya Chakula na yalifunguliwa rasmi tarehe 14 Novemba, 2024 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dustan Kitandula.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mhe. Dkt. Khalfan Haule ameipongeza Vi Agroforestry kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kituo hicho kuhusu kilimo mseto na kuwahamasisha wananchi kukitumia kituo hicho vizuri kujifunza na kuyafanyia kazi mafunzo hayo.
Aidha, Dkt. Haule amependekeza Wakala za Barabara kupanda miti pembezoni mwa barabara ambayo itakuwa ikitunzwa na wamiliki wa maeneo yanayopakana na barabara hizo ili kuongeza idadi ya miti inayopandwa hapa nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka amesema maonesho hayo yamefanyika kwa siku tatu na kwa muda huo wananchi wamejifunza namna bora ya kutumia eneo dogo kupata mavuno mengi.
Mhe. Chikoka amewataka wananchi wa Wilaya ya Musoma kutenga muda na kuja kujifunza katika kituo hicho na kuitumia elimu watakayoipata katika mashamba yao na kubadilisha maisha yao.
Akiwa katika maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa alipata nafasi ya kutembelea vipando, mabanda na kutoa zawadi kwa washindi mbalimbali waliofanya vizuri zikiwemo Halmashauri, taasisi, vikundi na shule za msingi na sekondari
Hafla ya kufunga maonesho hayo imehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara, Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Wakurugenzi wa Halmashauri, wataalamu wa kilimo, mifugo, uvuvi na kilimo mseto, na wananchi kutoka mikoa mbalimbali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa