Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amepokea awamu ya pili ya Madaktari Bingwa 63 wa Mama Samia na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuchangamkia fursa za uwepo wa Madaktari Bingwa kupata huduma za kibingwa katika maeneo yao.
Akizungumza katika mapokezi hayo, Mhe. Mtambi amesema Serikali imewasaidia wananchi na badala ya wagonjwa kwenda kwenye hospitali za rufaa ambazo zipo mbali kupata huduma za kibingwa, wanapata huduma za kibingwa na kibobezi katika maeneo yao baada ya Serikali kufanya maboresho makubwa katika sekta ya afya.
“Hii imewezekana kwa sababu Serikali imeboresha miundombinu na vifaa tiba na watumishi katika Hospitali za Halmashauri na vituo vya afya na kuwezesha madaktari bingwa kuweza kutoa huduma katika Hospitali hizo” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema madaktari hawa watatoa huduma katika Hospitali ya Manispaa ya Musoma, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Hospitali ya Nyamwaga, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Hospitali ya Wilaya ya Rorya.
Aidha, madakatari hao watatoa pia huduma katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Hospitali ya Manyamanyama (Bunda Mjini), Kituo cha Afya Ikizu na Kituo cha Afya Kasahunga vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Kwa mujibu wa Mhe. Mtambi magonjwa yatakayotibiwa na madaktari hawa ni magonjwa ya wanawake na uzazi, watoto na watoto wachanga, magonjwa ya ndani kama vile kisukari, presha na kadhalika, upasuaji na matatizo ya mfumo wa mkojo na magonjwa ya kinywa na meno.
Mhe. Mtambi ametoa rai kwa wataalamu wa afya wa Mkoa wa Mara kusimamia na kuratibu vizuri zoezi hili ili wananchi wenye changamoto waweze kupata huduma stahiki na kwa wakati na kwa kuzingatia maelekezo na miongozo ya Serikali.
Mhe. Mtambi amewakaribisha sana madaktari bingwa katika Mkoa wa Mara na kuwataka kabla ya kuondoka watembelea kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kula nyama choma na kichuri katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wizara ya Afya Dkt. Joakim Masunga ameeleza kuwa Halmashauri zote zimepangiwa Madaktari Bingwa na Wauguzi Bingwa watakaosaidia kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi kulingana na mahitaji.
Dkt. Masunga ameeleza kuwa madaktari hao wanatarajiwa kuanza kutoa huduma kuanzia leo hadi tarehe 16 Novemba, 2024 na wanategemewa kutumia muda wao kushughulikia matatizo mbalimbali ya wagonjwa.
Dkt. Masunga amesema madaktari hao bingwa wakiwa katika Hospitali hizo watawajengea uwezo watumishi wa sekta ya afya katika maeneo mbalimbali, watasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa na kuongeza mapato ya hospitali hizo.
Dkt. Masunga ameeleza kuwa madaktari hao watatoa huduma katika vituo hivyo kuanzia tarehe 11 Novemba, 2024 hadi tarehe 16 Novemba, 2024 na watafanya kazi katika muda wa kawaida wa kazi wa hospitali za Halmashauri na vituo vya afya.
Hafla mapokezi ya madaktari hayo imehudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Menejimenti ya Sektretarieti ya Mkoa wa Mara, Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma, Wakurugenzi wa Halmashauri, Timu ya Usimamizi wa Sekta ya Afya Mkoa wa Mara (RHMT) na Waganga Wakuu wa Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa