Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Wilaya ya Butiama baada ya Serikali kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT).
Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa miundombinu mtambuka wenye thamani ya shilingi bilioni tisa katika ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) na mkandarasi Shandong Hi-Speed Dejian Group Co. Ltd na Mshauri Mwelekezi Epitome Architects Limited Mhe. Mtambi amesema fursa zinazotokana na uwepo na Chuo hicho kwa Mkoa wa Mara ni nyingi.
“Niwaombe wananchi wa Mkoa wa Mara na Watanzania wote kwa ujumla, kuchangamkia fursa ya kuanzishwa kwa Chuo hiki kuwekeza katika biashara mbalimbali zitakazokuwa zinahitajika kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi na watumishi wanaotegemewa kuwepo katika Chuo hiki” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema kutokana maamuzi ya Serikali kukifanya Chuo hicho kibebe sehemu ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa Chuo hicho na ambacho amesema kitakapokamilika kitaleta mapinduzi makubwa ya kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Mara.
“Chuo hiki kinasadifu shabaha halisi ya kumuenzi Baba wa Taifa na kama Mkoa tunaishukuru Serikali kwa maamuzi yake ya kujenga Chuo hiki katika Mkoa wa Mara, huu ni mmoja kati ya miradi mikubwa ya kimkakati hapa nchini” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi amekipongeza Chuo kwa kujenga majengo na miundombinu mtambuka ambayo itaboresha zaidi eneo hilo na kuifanya miundombinu iliyokuwepo na inayoendelea kujengwa katika eneo hilo itumike kiurahisi zaidi na ujenzi utakapokamilika iweze kutoa huduma stahiki.
Mhe. Mtambi amewataka wakandarasi walioshinda zabuni mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya Chuo hicho kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili miundombinu inayojengwa iweze kutumika na kuwahakikishia kuwa Mkoa utatoa ushirikiano unaohitajika katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu na Mwenyekiti wa Baraza la MJNUAT Ndugu Philemon Luhanjo amesema Chuo hicho kitakapokamilika na kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wengi na hivyo kuleta matokeo chanya katika Mkoa wa Mara na kuwaomba wananchi kutumia fursa hiyo kuwekeza.
“Ninashukuru sana kwa ushirikiano ambao Chuo hiki unaupata kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama na viongozi wengine katika Mkoa wa Mara” amesema Ndugu Luhanjo na kuongeza kuwa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho inategemewa kukamilika mapema mwakani kama mikataba ya ujenzi inavyoonyesha.
Ndugu Luhanjo ameipongeza Menejimenti ya Chuo kwa usimamizi mzuri wa mikataba ya ujenzi na kuwezesha kufikia wastani wa asilimia 43 ya ujenzi wa majengo 15 ambayo ni sehemu ya miundombinu ya Chuo hicho katika Kampasi Kuu.
Ndugu Luhanjo ametumia nafasi hiyo kuwataka watumishi na viongozi wote wa Chuo hicho kutimiza wajibu wao kikamilifu kwani wamepata bahati ya kuwa katika waanzilishi wa Chuo hicho ili waweze kuandaa mazingira mazuri kwa watu wengi zaidi kujiunga na chuo hicho.
Ndugu Luhanjo amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa Chuo hicho kitafuatilia na kuhakikisha ujenzi wa miundombinu hiyo yote unafanyika kwa mujibu wa mkataba na makubaliano yaliyofikiwa.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lesakit Mellau ameeleza kuwa mradi wa miundombinu mtambuka ni sehemu ya mradi mkubwa wa shilingi bilioni 102.5 za mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambapo katika ujenzi wa majengo ya mradi huu umeanza na unaendelea vizuri.
“Katika mradi huo uliofadhiliwa na Benki ya Dunia, MJNUAT kimepata fedha ambazo ni sawa na asilimia 10 za fedha zote zilizotolewa kwa taasisi nyingine 22 za Elimu ya Juu hapa nchini, hili ni jambo la kujivunia sana” amesema Prof. Mellau.
Prof. Mellau ameeleza kuwa ujenzi wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia kwa sasa unaendelea vizuri na umefikia wastani wa asilimia 43 na Chuo kinategemea ujenzi wa miundombinu mtambuka pia utatekelezwa kwa muda uliopangwa na kukamilika ndani ya muda uliowekwa katika mkataba wake.
Prof. Mellau amesema ujenzi utakapokamilika Chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi hadi 4,500 kwa Kampasi Kuu, wanafunzi 600 katika Kampasi ya Oswald Mwang’ombe na wanafunzi 1,500 kwa Kampasi ya Tabora na kinatarajiwa kuwa na wastani wa watumishi 700.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi huo kutoka MJNUAT Mkadiriaji Majenzi (QS) Osward Bujiku ameeleza kuwa mradi huo ambao ni sehemu ya mradi mkubwa unafadhiliwa na Benki ya Dunia na unategemewa kutekelezwa kwa muda wa miezi kumi na utagharimu shilingi 9,093,848,880.98.
QS Bujiku ameeleza kuwa mradi wa miundombinu mtambuka utahusisha ujenzi wa mfumo wa maji na ufungaji wa mfumo wa maji taka, ujenzi wa miundombinu ya michezo, ufungaji wa mifumo ya umeme, ujenzi wa barabara za ndani na ujenzi wa miundombinu katika shamba la mfano la Chuo hicho.
Bwana Bujiku ameeleza kuwa miundombinu mingine itakayojengwa katika mradi huo ni lango kuu la kuingilia Kampasi Kuu ya Chuo hicho, ujenzi wa kichomea taka kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Chuo hicho ujenzi wa kingo za kulinda maeneo ya mabonde yoliyomo katika eneo hilo.
Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mhe. Ludovick Kaegele, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Butiama, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Prof. Agness Mwakaje, Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Mipango na Utawala Dkt. Abubakari Said Mgelwa, Menejimenti na watumishi wa Chuo hicho.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa