Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ametembelea kambi ya mazoezi ya Timu ya Biashara United na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo itakapokuwa inacheza na timu ya Tabora United tarehe 12 Juni, 2024 katika Uwanja wa Karume, Manispaa ya Musoma.
“Baada ya kuangalia mazoezi yao ninaamini kesho watafanya vizuri, wageni wategemee bakuri la kichuri…..Ninawaomba wananchi tujitokeze kwa wingi kuishangilia timu yetu uwanjani wakati inatoa dozi za kichuri kwa wapinzani wao” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ameipongeza timu hiyo kwa maandalizi mazuri ya mchezo huo na kuwataka wachezaji kucheza vizuri na kuifunga timu ya Tabora United na kuwaahidi kuwa atakuwepo uwanjani kuangalia michuano hiyo.
Amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo ili iingie kwenye michuano ya ligi kuu na kuweza kuzileta timu kubwa kucheza katika Uwanja wa Karume jambo ambalo litaibua fursa mbalimbali za kijamii na kibiashara katika Mkoa wa Mara.
“Nikiwaangalia hawa wachezaji ninauona ushindi mkubwa kesho, wananchi mje uwanjani muone timu yetu ikitoa kichuri kwa Tabora United na timu zote zitakazokuja kucheza michezo yake katika Uwanja wa Karume” amesema Mhe. Mtambi.
Kwa upande wake, Kocha ya Timu ya Biashara United Bwana Amani Josia amemshukuru sana Mkuu wa Mkoa kwa kuja kuitembelea kambi yao na kuwatia moyo wachezaji wa timu hiyo kabla ya mechi hiyo muhimu kwa timu yao.
Bwana Josia amesema wanategemea upinzani kuwa mkubwa kwa sababu timu pinzani inatoka ligi daraja la kwanza na kwa kupoteza mechi hiyo itakuwa haiwezi kucheza tena ligi kuu katika msimu ujao wa ligi.
Bwana Josia amesema wachezaji wa Biashara United wanajitoa kuhakikisha ushindi unapatikana katika mechi hiyo na mechi ya marudio ambayo inatarajiwa kuchezwa hivi karibuni.
Mechi ya Biashara United na Tabora United mechi ya mchujo (play offs) katika Ligi Kuu ya NBC ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kuamua timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania kwa msimu ujao na mchezo wa marudio baina ya timu hizi mbili unatarajiwa kufanyika tarehe 19 Juni, 2024.
Timu ya Biashara United inapambana kuwania kucheza ligi kuu baada ya kupita kwenye mchujo wa ligi ya Championship na kuwa miungoni mwa washindi wa ligi hiyo kutokana na kuwa na wachezaji ambao wameshawahi kucheza kwenye ligi kuu katika misimu iliyopita.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa