Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amefanya ziara katika Wilaya ya Bunda na kuzungumza na Waandishi wa Habari na wananchi kuhusu zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi wa Kata ya Nyatwali na kukagua vituo vya kujiandikishia kupiga kura katika daftari la mkazi.
Akizungumzia zoezi la wananchi kulipwa fidia Nyatwali, Mhe. Mtambi amewataka wananchi kuhakikisha baada ya kupokea fidia wanafanya maandalizi ya kuhama katika eneo hilo ili kujiepusha na madhara ya wanyama wakali na hususan tembo ambao wamekuwa wakiharibu mazao na kubomoa nyumba katika eneo hilo.
“Zipo taarifa za kuwepo kwa tembo wengi katika maeneo haya na siku sio nyingi kutakuwa na hatari kwa binadamu kuendelea kubakia katika maeneo haya, hameni haraka hawa wanyama wanajua mmeshalipwa” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema malipo kwa awamu ya kwanza yamekamilika leo na hatua itakayofuata ni malipo ya fidia kwa ajili ya makaburi na maeneo ambayo yanafanyiwa tathmini wakati huu na kuwahakikishia wananchi kuwa malipo hayo yataanza kufanyika hivi karibuni.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi kubomoa nyumba zao maeneo hayo na vitu wanavyodhani wanaweza kutumia katika ujenzi kwenye maeneo wanayohamia kama vile matofali, mabati, mbao na kadhalika Serikali imewaruhusu kuondoka navyo ili kuwasaidia katika ujenzi katika maeneo mapya wanakoenda kuanzaa maisha.
Mhe. Mtambi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele kwa malipo ya fidia za wananchi ili waweze kuondoka eneo hilo kuwaepusha na adha waliyokuwa wakiipata ya kuvamiwa mara kwa mara na wanyama wakali wakiwemo tembo.
Aidha, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bunda kuwachukulia hatua za kisheria watu wote wanaowaibia wananchi kwa kuwadai mikopo yenye riba kubwa iliyotolewa kinyume cha taratibu za kawaida za utoaji wa mikopo iliyotolewa na taasisi ambazo hazijasajiliwa kisheria kutoa mikopo kwa wananchi.
Mhe. Mtambi amewataka wananchi kukataa kulipa riba kubwa zinazotolewa na taasisi hizo na wanaowadai waende kwenye vyombo vya sheria ili kudai marejesho ya mikopo hiyo ambayo amesema imetolewa kinyume cha sheria.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amewahamasisha wawekezaji mbalimbali kuwekeza katika Mkoa wa Mara kutokana na fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo kwenye sekta ya utalii, madini na ziwa Victoria.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi Mhe. Mtambi amewataka wananchi kuchagua viongozi bora watakaowasaidia kuleta maendeleo na kufikisha kero zao kwa viongozi wa juu ili ziweze kutatuliwa kwa haraka na kuwataka wanaojiona wanasifa kugombea ili kuweza kuwatumikia wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Dkt. Vincent Naano Anney akizungumza katika eneo hilo amesema leo Serikali imekamilisha kulipa fidia kwa awamu ya kwanza katika eneo hilo na wananchi ambao fidia zao hazijafika wakati huu watalipwa hivi karibuni baada ya kufanyiwa uhakiki na maafisa kutoka Wizara ya Fedha.
“Maafisa kutoka Hazina wanategemewa kuwasili Wilaya ya Bunda kuanzia kesho na watu wote wenye matatizo ya tathmini na ambao hawajapewa malipo wafike hapa ili waweze kusikilizwa na maafisa hao ili malipo ya fidia zao yaweze kuandaliwa” amesema Mhe. Dkt. Anney.
Mhe. Dkt. Anney amewahakikishia wananchi wote wenye changamoto mbalimbali ambao zimesababisha wasipate fidia zao wakati huu kuwa Serikali itazitatua mapema iwezekanavyo ili kuweza kukamilisha zoezi hilo kwa haraka.
Serikali ilitangaza kuiunganisha Ghuba ya Speke (eneo la Kata ya Nyatwali) na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa GN Na. 269 ya mwaka 1974 na mwaka huu wananchi wa eneo hilo wanalipwa fidia kupisha shughuli za uhifadhi kuendelea katika eneo hilo.
Mhe. Mtambi akiwa katika Wilaya ya Bunda amefanya kikao cha ndani na Kamati za Usalama za Mkoa na Wilaya ya Bunda, maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa na Halmashauri za Wilaya ya Bunda na Mji wa Bunda na baadaye kukagua vituo vya kujiandikisha kupiga kura kwa ajili ya Serikali za Mitaa na kujionea hali halisi ya uandikishaji katika vituo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa