Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo amefunga kikao cha mwaka cha Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) Mkoa wa Mara na kuwataka Wakuu wa Shule kuhakikisha wanafunzi wao wote wanapata chakula cha mchana shuleni.
Mhe. Mtambi amezitaka shule kuhakikisha wazazi na walezi wote wanatimiza wajibu wao wa kuhakikisha watoto wanapata chakula na kama kuna changamoto Wakuu wa Shule waziwasilishe kwa viongozi ili kuweza kupata suluhu lakini wanafunzi wapate haki yao.
“Mkoa wa Mara hakuna mwanafunzi atayeshinda na njaa kwa kuwa mzazi au mlezi wake hataki kutimiza wajibu wake wa kumpatia chakula mtoto wake kwa ajili ya kula shuleni, tutawachukulia hatua” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema Mkoa wa Mara hautakubali ukatili huu kwa wanafunzi uendelee kwa kuwa wazazi hawataki kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao kula shuleni na kuwataka Wakuu wa Shule kutoa taarifa kwa viongozi kuhusu wazazi wote ambao wamekataa kutimiza wajibu wao wa kutoa chakula cha watoto wao.
Mhe. Mtambi amepiga marufuku shule kutoa chakula kwa baadhi ya wanafunzi na wengine kuwaacha kwa sababu wazazi ama walezi wao hawajachangia chakula na badala yake Wakuu wa Shule wawataarifu viongozi katika maeneo yao ili wawachukulie hatua wazazi ambao hawajachangia chakula kwa ajili ya watoto wao.
Kanali Mtambi amewataka Wakuu wa Shule za Sekondari kutumia vizuri fursa iliyotolewa na Taasisi ya Pamoja Tuwalishe kwa kujenga majiko na stoo kwa mujibu wa maelekezo ya taasisi hiyo ili shule zote za Mkoa wa Mara ziweze kupatiwa majiko banifu na sufuria zake ili kuleta uhakika wa wanafunzi wengi kupata chakula cha mchana shuleni.
Mhe. Mtambi ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha Wakuu wa Shule kuboresha taarifa zao na kuwahamasisha wanafunzi wenye umri wa miaka zaidi ya 17 kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura zoezi linaloendelea katika Mkoa wa Mara hadi tarehe 10 Septemba, 2024.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bwana Makwasa Bulenga amewataka Wakuu wa Shule kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya wakati wa ufunguzi wa kikao hicho.
Bwana Bulenga amewataka Wakuu wa Shule wanaporudi katika vituo vyao vya kazi baada ya kikao hicho waonyeshe mabadiliko katika usimamizi wa shule zao na hususan ujifunzaji na ufundishaji wa wanafunzi na walimu.
Bwana Bulenga amewataka Wakuu wa Shule ambao hawajahudhuria kikao hicho kutoa maelezo yao kuhusu sababu zilizowafanya kuacha kushiriki katika kikao hicho muhimu.
Kwa upande wake, Mwalimu Anna African Sarita Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kirumi katika Wilaya ya Butiama akitoa neno la shukrani kwa Mkuu wa Mkoa amesema walimu wanajitahidi kufuatilia wazazi na walezi wa wanafunzi kuchangia chakula cha wanafunzi mashuleni lakini wazazi wengi hawataki kuchangia kwa visingizio mbalimbali.
Mwalimu Sarita ameahidi kwa niaba ya Wakuu wa Shule wote kuwa wataongeza juhudi katika kuwafuatilia wazazi kuchangia chakula ili wanafunzi waweze kutumia muda mwingi wakiwa shuleni kujifunza ili kufaulu masomo yao.
Aidha, ameahidi kwa kutumia kamati za shule, Wakuu wa Shule watawahamasisha wazazi kuweza kutumia nishati safi na majiko banifu ili wanafunzi waweze kupikiwa chakula katika mazingira salama na bila kuharibu mazingira.
Kikao hicho cha siku mbili kimefanyika kuanzia jana na leo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Songe iliyopo Manispaa ya Musoma na kuwakutanisha Wakuu wa Shule za Sekondari 301 za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa