Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 13 Septemba, 2024 ameongoza hafla fupi ya kuutambulisha mradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) utakaotekelezwa katika vitongoji 148 katika Mkoa wa Mara na kuwataka wakandarasi kukamilisha miradi kwa wakati.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mtambi amemtaka Mkandarasi wa mradi huo Daimon Company Limited pamoja na wakandarasi wengine waliopewa zabuni za kutekeleza miradi mbalimbali ya Umeme katika Mkoa wa Mara kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
“Umeme ni maisha, umeme ni maendeleo, Mheshimiwa Rais amedhamiria kuwaletea umeme wananchi wa Mkoa wa Mara maisha bora na maendeleo kwa njanya nyingi ikiwemo umeme, mlioaminiwa na kupewa miradi hii hakikisheni mhakikishe mnafanya kazi kama inavyotakiwa” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema katika upande wa huduma za umeme Mkoa wa Mara upo vizuri ambapo vijiji vyote 459 vimepata huduma ya umeme, aidha, Mkoa una vitongoji 2,503 na kati ya hivyo vitongoji 899 tu havina umeme mpaka sasa na baadhi yake miradi ya ufungaji wa umeme inaendelea.
Mhe. Mtambi amesema mbali ya mradi mpya unaotambulishwa katika hafla hiyo, kuna miradi mingine inayoendelea katika Mkoa wa Mara kwenye vitongoji 470 yenye thamani ya shilingi bilioni 90 na kwa sasa miradi hii ipo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji wake.
“Huyu mkandarasi mpya anayetambulishwa leo yeye atafunga umeme kwenye vitongoji 148 na kwa kasi ninayoiona ni matumaini yangu kuwa muda sio mrefu vitongoji vyote vya Mkoa wa Mara vitakuwa na huduma ya umeme” amesema Mhe. Mtambi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Mhandisi Ernest Makare amesema wapo Mkoani Mara kwa ajili ya kuutambulisha mradi utakaotekelezwa katika vitongoji 148 na mkandarasi mzawa Daimon Company Limited ambao unaanza kutekelezwa rasmi kuanzia tarehe 13 Septemba, 2024.
Mhandisi Makare amesema katika mradi huo, mkandarasi anatarajiwa kujenga transforma 48 katika eneo la kilomita 296 ambazo zitawanufaisha wananchi zaidi ya 5000 kwa gharama ya bilioni 18.6 ambazo zitatumika katika kutekeleza mradi huo.
Mhandisi Makare amewathibitishia wadau walioshiriki katika hafla hiyo kuwa kuwa REA itamsimamia mkandarasi na kuhakikisha anatekeleza mradi huo kwa haraka ili wananchi waweze kupata huduma za umeme katika maeneo hayo.
Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na kuhudhuriwa na viongozi wa REA na TANESCO Mkoa wa Mara, mkandarasi na baadhi ya watumishi kutoka TANESCO, REA na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa