Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amefunga rasmi Mafunzo ya Operesheni Miaka 60 ya Muungano kwa mujibu wa sheria yaliyofanyika na katika kikosi cha 822 JKT Rwamkoma, Wilaya ya Butiama na kuwataka wahitimu kuyaishi kwa vitendo mafunzo hayo.
Akizungumza mara baada ya kukagua gwaride, kuangalia vikundi vya maonyesho na kutoa zawadi kwa wahitimu waliofanya vizuri katika vipengele mbalimbali, Mhe. Mtambi amewata wahitimu hao kutumia ujuzi na maarifa waliyofundishwa kwa faida yao na jamii kwa ujumla.
“Katika mafunzo haya mmejifunza mambo mengi sana ambayo mkiyaishi kwa vitendo yanaweza kubadilisha maisha yenu na maisha ya watu wengi wanaowazunguka, hivyo ni jukumu lenu kuyaishi mafunzo haya kwa vitendo” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kuzingatia mshikamano na upendo kwa watu wote bila kujali tofauti za kabila, dini na itikadi za kisiasa.
Mhe. Mtambi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo muhimu kwa maendeleo ya vijana na kuwapongeza vijana hao kwa uvumilivu na ustahimilivu uliowasaidia kukamilisha mafunzo yao.
Mhe. Mtambi amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kukiishi kiapo cha utii walichokitoa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuyaishi mambo manne ya kijana wa JKT waliyoyasoma katika kiapo chao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi 822 JKT Rwamkoma Kanali Gaudensia Joseph Mapunda ameeleza kuwa mafunzo hayo yaliyofungwa leo yameanza tarehe 19 Juni, 2024 na yamefanyika kwa wiki 12.
Akizungumza kabla ya kuwakaribisha viongozi kuongea, Kanali Mapunda amesema lengo la mafunzo hayo kwa vijana ni kuwajengea uwezo na kuwapa mafunzo ya uzalendo na utaifa.
Kanali Mapunda amesema jumla ya vijana 1,133 walipokelewa katika kikosi hicho wakati wa kuanza mafunzo ambapo vijana 1,122 wamehitimu mafunzo yao huku vijana wakiume 11 hawakufanikiwa kuhitimu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro.
Kanali Mapunda amewashukuru viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, viongozi wa kimila na dini, wazazi, walezi na wananchi waliojitokeza kushiriki katika ufungaji wa mafunzo hayo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kanali Amos Gerald Mollo amesema amewataka wazazi na walezi kuwaruhusu vijana kujiunga na mafunzo hayo ili kujenga Taifa lenye vijana waliotayari kulitumikia.
Kanali Mollo amewataka vijana waliohitimu mafunzo hayo kulinda afya zao kwa kula vyakula sahihi, kufanya mazoezi na kuepuka matumizi ya madawa ya kulevya na kuepuka makundi mabaya katika jamii.
Kanali Mollo amewataka wahitimu hao kusoma kwa bidi katika mafunzo ya vyuo wanayoenda na kuwa mfano bora katika kulitumikia Taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mhe. Moses Ludoviko Kaegele amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kwenda kupambana na umaskini kupitia mafunzo ya ujasiriamali waliyopata katika kikosi hicho.
Mhe. Kaegele amewataka vijana hao na wananchi waliohudhuria ufungaji wa mafunzo hayo kwenda kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ili kuwapata viongozi bora.
Wakisoma risala yao kwa mgeni rasmi, wahitimu wa kikosi hicho wamesema katika mafunzo hayo yamejifunza mambo mbalimbali ikiwemo uzalendo kwa Taifa, ujasiliamali, kilimo, ufugaji na kupata mafunzo ya awali ya kijeshi.
Wahitimu hao wameliomba JKT kuimarisha upatikanaji wa maji wakati wa mafunzo kwa kuweka matanki makubwa ya maji katika eneo hilo ili kupunguza changamoto ya kukosekana kwa maji.
Kikosi cha JKT 822 kilianzishwa mwaka 1970 baada ya kuhamisha kikosi cha JKT kilichokuwepo Mwanza na kwa sasa kipo katika eneo la Rwamkoma na kina ukubwa wa ekari zaidi ya 1,000 na kina vikosi viteule vinne ikiwa ni pamoja na Kiteule Kanda ya Ziwa (Mwanza), Kiteule Tarime, Kiteule Bulamba na Kiteule Nanenane katika eneo la Nyakabindi Mkoa wa Simiyu.
Ufungaji wa mafunzo hayo umehudhuriwa pia na Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi, Kamati ya Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Butiama, viongozi wa Halmashauri ya Butiama, Chifu Japhet Wanzagi kiongozi wa Kabila la Wazanaki, viongozi wa vyama vya siasa, dini na vijiji vinavyoizunguka JKT Rwamkoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa