Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao cha wadau wa uchaguzi kuhusiana na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 katika ukumbi wa Uwekezaji na kuwataka wadau wa uchaguzi kuhakikisha kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika kwa amani na utulivu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amewataka wadau wote kushiriki kikamilifu katika kuwahamasisha wananchi kushiriki katika matukio muhimu ya uchaguzi kwa amani na kufuata miongozo inayotolewa na wasimamizi wa uchaguzi.
“Katika uchaguzi huu tunahitaji amani na utulivu, vyama na wagombea wanadi sera zao na kuwashawishi wananchi wawachague na Serikali ya Mkoa tutahakikisha tunaweka mazingira mazuri ya uchaguzi” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema zoezi la uandikishaji wa wapiga kura litafanyika kuanzia tarehe 11 hadi 20 Oktoba, 2024 na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili wapate haki ya kupiga na kupigiwa kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa maana wasipojiandikisha hawataweza kupiga kura.
Kanali Mtambi amesema sifa za mtu anayepaswa kujiandikisha ni; awe raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi, mkazi wa Mtaa, Kijiji au Kitongoji ambapo uchaguzi unafanyika na kuongeza kuwa orodha ya wapiga kura itabandikwa kwenye mbao za matangazo na Msimamizi wa Uchaguzi tarehe 21 Oktoba, 2024 ambapo watakaoonekana kwenye orodha hiyo ndio watakaoruhusiwa kupiga kura.
Mhe. Mtambi amesema zoezi la kuchukua na kurejesha fmu za kugombea nafasi za uongozi litafanyika tarehe 01-07 Novemba, 2024 na kuzitaja nafasi zonazogombewa kuwa ni Mwenyekiti wa Mtaa, Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (kundi mchanganyiko) na kundi la wananwake kwa Halmashauri za Miji na Manispaa.
Kwa Halmashauri za Wilaya, nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti wa Kijiji, Wenyeviti wa Vitongoji vilivyomo katika eneo la kijiji, wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi mchanganyiko) na kundi la wanawake.
Mhe. Mtambi amesema zoezi la uteuzi wa wagombea litafanyika tarehe 8 Novemba, 2024 na viongozi wa vyama vya siasa wanatakiwa kuwasilisha ratiba ya mikutano ya kampeni tarehe 14 Novemba, 2024 na kampeni za uchaguzi zitafanyika tarehe 20 Novemba, 2024 hadi tarehe 26 Novemba, 2024.
Mhe. Mtambi amezitaja sifa za mpiga kuwa kuwa ni Raia wa Tanzania, mwenye umri wa miaka 18 au zaidi, mkazi wa Mtaa, Kijiji, au Kitongoji ambapo uchaguzi unafanyika, aliyejiandikisha kupiga kura katika Mtaa, Kijiji, au Kitongoji chake.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi Mkoa wa Mara Bwana Dominicus Lusasi amesema Mkoa wa Mara una jumla ya tarafa 20, kata 178, mitaa 242, vijiji 458 na vitongoji 2,502, Wilaya sita na Halmashauri tisa.
Bwana Lusasi amesema Mkoa wa Mara unatarajiwa kuwa na wapiga kura 1,111,963 kulingana na takwimu Sensa ya Watu na Makazi yam waka 2022 zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
Bwana Lusasi amesema wakati wa uchaguzi Mkoa utakuwa na vituo vya uandikishaji 2,854 ambapo kati ya hivyo vituo 1,782 vipo kwenye majengo ya umma na vituo 1,065 havipo kwenye majengo ya umma na mkoa unatarajia kuwa na vituo vya kupigia kura 3,053 hii ni kutokana na ongezeko la vituo kwenye Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Kauli Mbiu ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 ni “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi”.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wazee wa kimila na machifu, Wakuu wa Idara na Vitengo vya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, mashirika yasiyo ya kiserikali, waratibu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa