Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 4 Julai, 2024 amefanya ziara katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na kuwataka wachimbaji wadogo wa mgodi wa Kinyambwiga uliopo katika Mtaa wa Stooni, Kata ya Guta kuungana katika vikundi vya uzalishaji mali.
Akizungumza katika maeneo ya wachimbaji hao na katika mkutano wa hadhara Mhe. Mtambi amewataka wachimbaji hao kuungana na kuunda vikundi vya uzalishaji mali ili waweze kunufaika na usaidizi wa Serikali na wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Mara.
“Mkiungana na kuwa na uongozi wenu itakuwa rahisi kwenu katika kufanya majadiliano kama kundi na kunufuika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo imedhamiria kuwasaidia wachimbaji wadogo kuboresha shughuli zao” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema uchimbaji mdogo wa madini ni ajira rasmi inayotambulika na Serikali kama zilivyo ajira nyingine na kumwagiza Kamishna Msaidizi wa Madini Mkoa wa Mara kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo mgodini hapo ili waweze kujua Sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazowaongoza katika uchimbaji wa madini.
Mhe. Mtambi amemtaka Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara kujenga kituo cha polisi katika mgodi huo kwa kushirikiana na wadau wanaofanya shughuli zao katika mgodi huo ili kuimarisha usalama wa watu na mali zao katika mgodi huo.
Aidha, amemuagiza Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuongeza transforma na usambazaji wa huduma za umeme katika eneo hilo baada ya kutaarifiwa kuwa transforma iliyopo imezidiwa nguvu na kwa sasa hawawaunganishii watu wapya umeme ili kuwasaidia wachimbaji kupata umeme katika shughuli zao.
Mhe. Mtambi amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kuongeza watumishi na dawa katika Zahanati ya Kinyambwiga na kumhamishia Afisa Afya katika eneo hilo na kupeleka ramani ya Shule ya Sekondari ili wananchi waweze kuanza kujenga Sekondari yao katika eneo hilo.
Kanali Mtambi amewataka wananchi wa eneo hilo kuwaheshimu na kuwasikiliza viongozi na kutoa taarifa kuhusu matukio mbalimbali ya kihalifu na ajali yanayotokea katika maduala na maeneo ya uchimbaji .
Akiwa eneo hilo, Mkuu wa Mkoa alisikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitolea ufafanuzi na maelekezo kwa viongozi wa ngazi ya Wilaya na Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya, Menejimenti ya Halmashauri ya Mji wa Bunda, mameneja wa Wilaya wa taasisi za umma na baadhi ya maafisa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Kabla ya kutembelea mgodi huo, Mkuu wa Mkoa alitembelea ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bunda na kuzungumza na viongozi kabla ya kuelekea Kinyambwiga kukagua mgodi na kuzungumza na wananchi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa