Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 14 Novemba, 2024 amemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufunga Kongamano la Fursa za Kiuchumi kwa vijana wa mikoa ya Mara, Simiyu na Mwanza lililofanyika katika Hoteli ya CMG, Mjini Tarime na kuwataka vijana kushiriki katika masuala ya uchaguzi.
“Tunashukuru kuwa vijana wengi mmejiandikisha katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, ninawaomba mjitokeze kugombea nafasi mbalimbali na kupiga kura katika chaguzi hizi ili kuwachagua viongozi bora” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema kujiandikisha tu bila kushiriki kupiga kura tarehe 27 Novemba, 2024 haitakuwa na maana yoyote ile na kuwataka kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi watakaosimamia maendeleo ya maeneo yao.
Mhe. Mtambi amewataka vijana kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazoendelea kuzifanya katika sekta mbalimbali hapa nchini na kuwataka vijana kumuunga mkono kwa kufanya kazi kwa bidi ili kujiletea maendeleo yao.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka amesema sifa kubwa ambayo vijana wanapaswa kuwa nazo ni kujiamini, uthubutu na kuchungulia fursa na kuzifanyia kazi na amewapongeza vijana wote walioshiriki katika kongamano hilo.
Mhe. Chikoka amesema mwaka huu uchaguzi upo mikononi mwa vijana ndio watakaoamua hatma ya jamii zetu kwa kwenda kupiga kura na kuhakikisha amani na utulivu katika maeneo yote ili kusiwe na hofu ya wananchi kujitokeza kwenda kupiga kura.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tarime Mjini Mhe. Michael Kembaki amesema Chama cha Mapinduzi kimejipanga vizuri katika Mkoa wa Mara na kina uhakika wagombea wake wengi watashinda katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu.
“Tutapita Mtaa kwa Mtaa, Kijiji kwa Kijiji, Kitongoji kwa Kitongoji na nyumba kwa nyumba kufanya kampeni na kuwahamasisha watu waliojiandikisha kupiga kura” amesema Mhe. Kembaki.
Mhe. Kembaki amewataka vijana hao kukisaidia Chama kufanya kampeni na kuwahamasisha vijana wenzao kuwachagua viongozi bora watakaosaidia kuleta maendeleo katika maeneo yao.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa