Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo tarehe 14 Novemba, 2024 amemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Kongamano la Fursa za Kiuchumi kwa vijana wa Mikoa ya Mara, Simiyu na Mwanza lililofanyika katika Mji wa Tarime na amewataka vijana kuchangamkia fursa.
“Niwatake vijana kuchangamkia fursa mbalimbali mlizojifunza leo na fursa nyingine zilizopo hapa nchini ili kuweza kubadilisha maisha yenu na maisha ya familia zenu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema Serikali imefadhili programu mbalimbali za kuendeleza ujuzi wa vijana zenye lengo la kuwafanya vijana waweze kuajiriwa na kujiajiri ikiwa ni pamoja na kuwapeleka katika mafunzo nje ya nchi ili kupata ujuzi stahiki na hususan katika kilimo cha umwagiliaji.
Mhe. Mtambi amesema kwa kutambua umuhimu wa mitaji, Serikali imeweka mfumo rahisi wa kutoa mikopo kwa vijana katika vikundi na kijana mmoja mmoja kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zote hapa nchini.
Mhe. Mtambi amewataka vijana kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo na uwepo wa mitaji kupitia mikopo yenye masharti nafuu ili kuweza kujikomboa kiuchumi.
Mhe. Mtambi amewataka vijana kushiriki katika kupiga vita matumizi ya madawa ya kulevya na badala yake watumie maarifa na elimu waliyoipata katika kongamano hilo kuboresha maisha yao kiuchumi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Salvio Kapinga amesema Serikali ya awamu ya Sita imewekeza sana kwa vijana na imeandaa mazingira wezeshi na kutoa fursa nyingi kwa makundi mbalimbali ikiwemo vijanana kuwataka vijana kuchangamkia fursa hizo.
“Katika Wizara ya Nishati, tunayo mikopo ya kuanzisha vituo vidogo vya mafuta vijijini zinazotolewa na Wakala wa Nishati Vijiji (REA) na mikopo hii unaweza kuiomba binafsi au kwenye vikundi” amesema Mhe. Kapinga.
Mhe. Kapinga amewataka vijana kuchangamkia fursa na kuongeza kuwa hakuna mtu atakayekuja kuwatoa katika umaskini bila ya wao kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao yanayowazunguka na kuwataka kujifunza mambo mbalimbali ili kupanua uelewa wao.
Mhe. Kapinga amesema hivi sasa Serikali imeendelea kusambaza umeme katika vijiji na vitongoji ambapo hadi sasa bado kuna vijiji 70 nchi nzima ambavyo havijafikiwa na vitongoji vingi, lakini ni mpango wa Serikali kuhakikisha vitongoji vyote vinafikiwa ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Mbunge wa Vijana kutoka Mkoa wa Mara Mhe. Juliana Masaburi ameeleza kuwa lengo la kuandaa kongamano hilo lilikuwa ni kuwawezesha vijana kutambua fursa mbalimbali zilizopo Serikalini katika sekta mbalimbali ili waweze kuzifanyia kazi.
Mhe. Juliana amesema Serikali imeweka fursa mbalimbali za kuwawezesha vijana lakini hata hivyo vijana hawana uelewa wa fursa nyingi zilizopo na hivyo hawazichangamkii kwa sababu hawazijui na hawajui wanawezaje kuzipata.
“Mfano katika mfumo wa NEST (Mfumo wa Manunuzi Serikalini) Serikali imetenga asilimia 30 ya manunuzi yote ya umma kwenda kwa vijana, lakini vijana wenyewe hawajui kuhusu fursa hii ya kufanya biashara na Serikali” amesema Mhe. Masaburi.
Mhe. Masaburi amesema Serikali pia imeanzisha mifuko mingi ya uwezeshaji kwa vijana lakini na mifuko hii yote inazo fursa mbalimbali lakini fursa hizi haziwafikii walengwa kwa sababu walengwa ambao ni vijana hawana taarifa sahihi ya auwepo wa fursa hizi na namna ya kuzipata.
Mhe. Masaburi ameomba kuwepo na Ofisi mahususi ya Waziri Mkuu katika Mikoa ili kuwaelezea vijana namna ya kupata fursa mbalimbali zinazoratibiwa na taasisi za Serikali na ameiomba taasisi kuboresha tovuti zao ili wananchi waweze kupata taarifa mbalimbali kiurahisi zaidi.
Akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Meja Edward Gowele amewataka vijana kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao katika sekta za kilimo, madini, mifugo, uvuvi, usafilishaji na kadhalika.
“Mkijitambua na kutumia vizuri fursa zilizopo katika maeneo yetu na miongozo ya Serikali katika matumizi ya fursa hizo mnaweza kufanya vizuri katika maisha yenu” amesema Mhe. Gowele.
Mhe. Gowele ameeleza kuwa lengo la kongamano hili ni kuwajengea uwezo vijana kuhusiana na fursa hizo ili waweze kuzitumia kubadilisha maisha yao na jamii kwa ujumla na kuongeza kuwa vijana ni nguzo muhimu ya Taifa ya leo na hivyo wanajengewa uwezo ili wawe watu wenye manufaa katika jamii.
Mhe. Meja Gowele ametumia fursa hiyo kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika hapa nchini tarehe 27 Novemba, 2024 ili kuwachagua viongozi bora na sio bora viongozi.
Kwa upande wake Afisa Vijana kutoka Sektretarieti ya Mkoa wa Mara Bwana Fidel Baragaye akiwasilisha mada kuhusu fursa za kiuchumi zilizopo katika Mkoa wa Mara amewataka vijana kutumia fursa mbalimbali zilizowasilishwa katika kongamano hilo.
Bwana Baragaye amewataka vijana kujiunga kwenye vikundi ili kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri na kuongeza kuwa katika awamu ya kwanza Mkoa wa Mara umetenga jumla ya shilingi bilioni 2.4 ambazo zitatolewa kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu
Bwana Baragaye ametoa mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambapo ameeleza kuwa kwa awamu ya kwanza Halmashauri hiyo imetenga shilingi milioni 500 kwa vikundi hivyo, kwa kuzingatia mfumo wa 4 4 2 ambapo itatoa shilingi milioni 200 kwa vijana, milioni 200 kwa wananwake na shilingi milioni 100 kwa watu wenye ulemavu.
Bwana Baragaye ameeleza kuwa sifa za vijana kupata mikopo ni pamoja na kutengeneza kikundi cha vijana wa Kitanzania, kikundi hicho kiwe kimesajiriwa na Halmashauri husika, kikundi kinaweza kuwa na mradi au kinatarajia kuanzisha mradi, kikundi kiwe na akaunti ya benki, idadi ya wanakikundi ni kuanzia watu watano na kuendelea.
Bwana Baragaye amesema Serikali imefanya maboresho na kwa sasa ili kujiunga na vikundi vijana wanaotakiwa kupata mikopo ni wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi miaka 45 na maboresho mengine ni kwa sasa kijana mmoja anaweza kuandika mradi wake na akapata mkopo wa Halmashauri sio lazima ajiunge kwenye kikundi.
Bwana Balagaye amesema mikopo inayotolewa ni kuanzia shilingi 500,000 hadi milioni 100 kwa kikundi na marejesho ya mkopo yanategemea makubaliano kati ya Halmashauri husika na wakopaji.
Akizungumza katika kongamano hilo, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Biashara na Uwekezaji Bwana Gambales Timotheo amewataka vijana kubadilisha mitazamo yao katika maisha yao na kuwaasa vijana kuwajibika na kuyapambania maisha yao.
Bwana Timotheo amesema kijana akijishughulisha na kujipatia shughuli zake za maendelo atakuwa amejiajiri yenye mwenyewe na kuwataka vijana kujenga tabia ya uwajibikaji na uaminifu ili kuweza kuaminiwa na kupata manufaa ya mikopo inayotolewa.
Bwana Timotheo amewataka vijana kuwaza aina ya biashara, masoko ya biashara hiyo, mtaji wa biashara hiyo na namna ya kuupata mtaji wa kuanzisha biashara hiyo na kujua muda wa kufanya biashara kulingana na aina ya biashara.
Aidha, Bwana Timotheo amewataka vijana kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao ili kujenga na kuboresha maisha yao na familia zao.
Kongamano la Fursa za Kiuchumi kwa vijana limeandaliwa na Mbunge wa Viti Maalum Vijana Mhe. Juliana Masaburi na kudhaminiwa na taasisi mbalimbali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa