Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Afred Mtambi tarehe 25 Aprili, 2024 amewaongoza wananchi wa eneo la Nyasho, Manispaa ya Musoma katika kufuatilia hotuba ya Miaka 60 ya Muungano iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa hotuba hiyo, Mhe. Mtambi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kujivunia mafanikoa ya Muungano kwa kuwa Mwasisi wa Muungano Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye pia ni Baba wa Taifa letu ametokea Mkoa wa Mara.
“Tunatakiwa tutembee kifua mbele, tuwe na fahari, tujisikie vizuri sana kwa sababu mwasisi mmoja wapo wa Muungano ni Mwanamara----kwa hiyo Mara ni waasisi wa Muungano wa Tanzania, sisi ni kati ya Watanzania wanaotakiwa kutembea kifua mbele kujivunia Muungano wetu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema Mkoa wa Mara ni waasisi wa Muungano wa Tanzania na kama Watanzania wengine ni sehemu ya mafanikio ya miaka 60 ya Muungano na kuwataka wananchu kuendelea kuuenzi, kuulinda na kuuishi muungano wetu kwa vitendo.
Mhe. Mtambi amekemea vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na kukatana mapanga au kuchomana visu katika mambo ambayo yanaweza kuzungumzika au kutafutiwa suluhu nzuri ikiwemo kushtakiana kuliko kuumizana.
“Miaka sitini ya Muungano, Mara uoga sasa basi, pamekuwa na matukio mengi Mkoa wa Mara ya watu kupigana visu, mapanga na vitu vyenye ncha kali, huo ni uoga, mwanaume unapigana kwa panga? Ukihitilafiana na mwenzako, hatua ya kwanza ni kumfuata na kuzungumza nae sio kumchoma mwenzako na visu na kukimbia, huo ni uoga” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ametumia muda huo pia kujitambulisha kwa wananchi wa Kata ya Nyasho walioungana nae kufuatilia hotuba hiyo na kuwaomba ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli zake na kuwaahidi milango ya ofisi yake ipo wazi wakati wowote.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Dkt. Khalfan Haule ameeleza kuwa Mkoa wa Mara umepiga hatua kubwa sana katika miaka 60 ya Muungano ambapo kabla ya Muungano Mkoa ulikuwa na Wilaya mbili tu Musoma na Tarime lakini kwa sasa Mkoa una Wilaya sita na Halmashauri tisa.
Dkt. Haule amesema kwa sasa Serikali imeshatoa fedha za ujenzi wa soko la kisasa la Mkoa katika eneo la Nyasho na Stendi ya Mkoa katika eneo la Bweri ambapo miradi hiyo itakapokamilika itabadilisha sana madhari na uchumi wa Wilaya ya Musoma.
“Thamani ya miradi hii ni bilioni 14, wataalamu wameanza kupita na hatua mbalimbali za kuwapata wakandarasi wa kutekeleza miradi hiyo zinaendelea na tayari tumeshakutana na wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo haya na kuzungumza nao” amesema Dkt. Haule.
Kwa mujibu wa Dkt. Haule wafanyabiashara wa sasa wa eneo la Nyasho watahamishwa kupisha ujenzi wa mradi huo na baada ya ujenzi kukamilika watarudishwa katika soko hilo kuendelea na biashara zao katika mazingira mazuri zaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Benedict Magiri ameeleza kuwa kuna mafanikio makubwa sana katika Mkoa wa Mara tangu waasisi wa Muungano walipoiunganisha Tanzania kuwa nchi moja hadi leo hii.
Mhe. Magiri ameeleza kuwa Wanamara kama watanzania wengine tuna kila sababu ya kujivunia kuwa Watanzania kwa kuwa tuna amani na uhuru wa kutosha katika mkoa wetu na nchi yetu unaotusaidia kufanya shughuli za maendeleo.
Bwana Magiri amesema kwa kipindi hichi chote cha Muungano, kuna maboresho makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, usafiri, utawala na kadhalika. Maendeleo ni makubwa sana katika Mkoa wa Mara, pamoja na kuwepo na changamoto ndogondogo zinazoendelea kutatuliwa na Serikali, wananchi wenyewe na wadau wa maendeleo.
Shughuli hiyo ilihudhuriwa pia na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Musoma, watumishi wa umma kutoka taasisi zote zilizopo Manispaa ya Musoma, wanachama wa Chama cha Mapinduzi na wananchi wa Kata ya Nyasho.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa