Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameshiriki katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Televisheni ya Clouds kuhusiana na huduma za maji na kusema kuwa Serikali imewekeza shilingi bilioni 497 katika miradi mbalimbali ya maji katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika kipindicha 360 kilichorushwa mubashara kutokea Chujio la Maji la Bukanga, Manispaa ya Musoma, amesema tangu iingie madarakani tayari Serikali ya Awamu ya Sita imetoa shilingi trilioni 1.22 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Mara na kati ya miradi hiyo uboreshaji wa huduma za maji umepewa kipaumbele.
“Uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ni mkubwa sana ukilinganisha na uwekezaji ambao umefanyika katika uboreshaji wa huduma za maji tangu nchi ilipopata uhuru” amesema Kanali Mtambi na kuongeza kuwa hivi sasa kila Wilaya ina mradi mkubwa wa maji unaoendelea.
Mhe. Mtambi amesema tangu nchi ilipopata uhuru mpaka mwaka 2021 Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani, upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Mara ulikuwa na wastani wa asilimia 59.1 lakini kwa sasa ni wastani wa asilimia 74 na kuongeza kuwa miradi inayoendelea ikikamilika Mkoa utakuwa na hali nzuri zaidi katika upatikanaji wa maji.
Mhe. Mtambi ameitaja miradi mikubwa inayotekelezwa kuwa ni pamoja na mradi wa Rorya- Tarime- Sirari unaotoa maji Ziwa Victoria na kwenda katika Wilaya za Tarime na Rorya wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 134 na mradi mwingine ni mradi wa Maji wa Mgango- Kiabakari- Butiama unaotoa maji Ziwa Victoria na kusambaza katika vijiji 39 vya Wilaya za Butiama, Bunda na Musoma kwa gharama ya shilingi bilioni 70.5.
Mhe. Mtambi amesema kuwa hali ya upatikanaji wa maji kwenye vijiji ni asilimia 74.6 wakati mijini ni asilimia 76 na kuongeza kuwa ni matumaini yake kuwa mwishoni mwa 2025 miradi mingi inayoendelea itakuwa imekamilika na Mkoa wa Mara utafikia lengo la Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 katika upatikanaji wa maji.
Mhe. Mtambi amesema kwa sasa sehemu kubwa ya wananchi wa Mkoa wa Mara wanapata maji safi, salama na ya uhakika na hivyo kutumia muda mwingi kutekeleza majukumu mengine ya kiuchumi badala ya kutafuta maji.
Wakati huo huo, Mhe. Mtambi amewahamasisha watu wanaotaka faida katika uwekezaji kuwekeza mitaji yao katika katika fursa mbalimbali zilizopo katika Mkoa wa Mara.
Ameyataja maeneo yenye fursa nyingi za uwekezaji kuwa ni Ziwa Victoria katika ufugaji wa samaki katika vizimba, uwekezaji katika fukwe, usafirishaji wa majini, utalii wa kwenye maji na kuanzisha migahawa inayotembea na uwekezaji katika sekta za ufugaji.
Akizungumzia kuhusu madini, Mhe. Mtambi amesema katika Mkoa wa Mara kila Wilaya ina migodi ya madini na madini yanayopatikana kwa wingi ni dhahabu, shaba na mengine na kuwataka wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hizo.
Mhe. Mtambi amesema wananchi wa Mkoa wa Mara ni watu hodari sana na katika wafanyabiashara wakubwa wa nchi hii na hususan mikoa ya Kanda ya Ziwa, wananchi wa Mkoa wa Mara wanafanya vizuri sana katika nyanja zote.
Wengine walioshiriki kipindi hicho ambacho kilikuwa kinazungumzia huduma za maji katika Mkoa wa Mara ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka, Meya wa Manispaa ya Musoma Mhe. Patrick William Gumbo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Musoma Mhe. Benedict Magiri na viongozi wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa