Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Mkoa wa Mara yaliyofanyika katika Hoteli ya Afrilux ,Manispaa ya Musoma na kuwataka Waandishi wa Habari kutumia maarifa yao na ubunifu kuutangaza Mkoa wa Mara.
Akizungumza wakati wa kufunga maadhimisho hayo, Mhe. Mtambi amesema taswira ya Mkoa wa Mara iliyopo nje ya Mkoa ni tofauti na hali halisi iliyopo ndani ya Mkoa wa Mara na kwamba kuna mambo mengi mazuri yaliyopo lakini hayapewi kipaumbele na Waandishi wa Habari na vyombo vya habari hapa nchini.
“Mkoa wa Mara una mambo mengi mazuri ambayo hayaandikwi ipasavyo au hayaandikwi kabisa kama vile uwepo wa asilimia kubwa ya Ziwa Victoria, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, madini, wasomi na viongozi kutoka Mara, wakulima na wafugaji wazuri hayapewi kipaumbele kwenye vyombo vyetu vya habari” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi amewataka Waandishi wa Habari kuandika habari kwa kuzingatia weledi na maadili ya uandishi wa habari na uhalisia uliopo na sio kutoa habari mbaya tu kila wakati ambazo amesema hazijengi taswira nzuri ya Mkoa wa Mara kwa wadau wake waliopo ndani na nje ya Mkoa wa Mara.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka Watendaji Wakuu wa Taasisi na Viongozi wa Mkoa wa Mara kutoa ushirikiano kwa waandishi wa Habari ili waweze kupata taarifa kwa urahisi na kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao.
Kanali Mtambi ameipongeza Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mara kwa kazi nzuri inayoifanya na kumuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma kuitafutia kiwanja Klabu hiyo ili iweze kujenga ofisi na kuahidi kuwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara itachangia katika ujenzi wa ofisi ya Klabu hiyo.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka waandishi kutumia vizuri uhuru waliopewa na kuongeza kuwa pamoja na Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwapa uhuru wa kutosha, uhuru huo umeambatana na wajibu kwa Waandishi wa Habari kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, miongozo na taratibu za nchi.
Mkuu wa Mkoa pia amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi wa Kata ya Nyatwali Wilaya ya Bunda wanahama katika eneo hilo kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA).
Akisoma risala ya Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, Kaimu Mwenyekiti wa Klabu hiyo Bwana Raphael Okello amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa ushirikiano mkubwa aliouonyesha kwa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara na hususan kushiriki katika maadhimisho hayo.
Bwana Okello ameeleza kuwa Klabu yao imeanza mchakato wa kutafuta kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi lakini inakabiliwa na uhaba wa fedha na kuiomba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na wadau wengine kuwasaidia kununua kiwanja hicho.
Bwana Okello amezitaja baadhi ya changamoto kuwa ni baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali wamekuwa hawatoi ushirikiano kwa Waandishi wa Habari katika kutekeleza majukumu yao jambo ambalo linakiuka uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa habari.
Ameitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya Waandishi wa Habari kukosa bima ya afya na hivyo kuwawia vigumu kupata matibabu pindi wanapokuwa wameugua.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa pia na wadau mbalimbali wakiwemo Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Manispaa ya Musoma, Mgodi wa Barrick North Mara, Wakala wa Maji Vijijini na Mijini (RUWASA), Wakala wa Misitu (TFS), viongozi wa vyama vya siasa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Kitaifa Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yalifanyika Mkoani Dodoma tarehe 03 Mei, 2024 na Mgeni Rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa (Mb.).
Kauli mbiu ya maadhimisho haya mwaka huu ilikuwa “Uandishi wa Habari na Changamoto za Mabadiliko ya Tabia Nchi”.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa