Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao kazi kati ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) na viongozi wa vyama vya Siasa Mkoa wa Mara kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji na kuwataka kufanya kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kiustaarabu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amevitaka vyama vya siasa kufanya kampeni za kiustaarabu na kuhakikisha kuwa siasa za maji taka, mifarakano, ukabila na kujenga chuki zisiwe Sehemu ya Mkoa wa Mara.
“Kamati ya Usalama ya Mkoa tumejipanga kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu na mtu yeyote anayejipanga kuharibu uchaguzi kwa namna yoyote ile atachukuliwa hatua kali za kisheria” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuwahamasisha wananchi wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura tarehe 27 Novemba, 2024 ili kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa viongozi bora watakaowaletea maendeleo yao.
Kanali Mtambi amesema wananchi wa Mkoa wa Mara ni wasikivu ni wastaarabu na wanautulivu wa kisiasa na amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara wasitumike na wanasiasa uchwara wanaotaka kuwatumia kuharibu uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mhe. Mtambi amevitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa vitakavyoshindwa katika uchaguzi huu kurudi na kujipanga upya ili kuweza kupanga mipango mizuri ya kushinda katika chaguzi zijazo.
Kwa upande wake, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mara Mohamed Sharif akitoa mada kwenye kikao hicho ameviomba vyama vya siasa kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU kwa kutoa taarifa wanapobaini matukio yanayohisiwa kuwa ya rushwa.
“Kwa ushirikiano wetu tukiamua kwa pamoja kuna kuwa hamna rushwa au inaweza kuzuiwa kwa kiasi kikubwa amesema Bwana Sharif na kuwataka viongozi hao kuwapa elimu wanachama na viongozi wao ili kuweza kuizuia rushwa ndani nan je ya vyama vyao.
Bwana Sharif ameeleza kuwa malengo makubwa ya taasisi hiyo ni kuchochea maendeleo ya utawala bora na kuzuia na kupambana na rushwa hapa nchini na kuongeza kuwa kutokana na malengo hayo, taasisi hiyo inahusika na kufuatilia mwenendo mzima wa uchaguzi.
Bwana Sharif ameeleza kuwa wakati wa uchaguzi wananchi wanatakiwa kutumia fursa hiyo kutafakari changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ili waweze kujua namna ya kuzitatua na kumtafuta mtu atakayewaongoza katika kuleta maendeleo yao.
Bwana Sharif amesema katika utafiti wa TAKUKURU katika changuzi za mwaka 2014, 2019 na 2020 umebaini kuwa wakati wa uchaguzi kunakuwepo na matatizo ya kimaadili ambapo kuna kuwa na matukio ya rushwa, kampeni kabla ya ratiba rasmi ya kampeni, lugha za matusi, kejeli na kashfa na tatizo la vyama kuingilia kampeni za vyama vingine vya siasa.
Bwana Sharif amebainisha kuwa TAKUKURU imebaini viashiria mbalimbali vya rushwa na mianya ambayo inatumika katika kutoa na kupokea rushwa nyakati za uchaguzi na taasisi hiyo imejipanga kikamilifu kuweza kufuatilia uchaguzi katika maeneo mbalimbali.
Kamanda wa TAKUKURU amewataka viongozi wa vyama vya siasa kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za matukio yenye viashiria vya rushwa ili TAKUKURU iweze kufuatilia matukio hayo na kutoa elimu kwa viongozi wengine na wanachama wa vyama vyao kuhusiana na masuala ya rushwa katika uchaguzi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara, Menejimenti ya Sekrearieti ya Mkoa wa Mara na Maafisa kutoa TAKUKURU.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa