Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 13 Agosti, 2024 amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Majimoto kushughulikia mgogoro kati ya mgodi wa madini na wananchi na kuunda kamati itakayopitia na kufuatilia uhalisia wa taarifa za mgogoro huo na kutoa mapendekezo.
Akizungumza baada ya kukagua eneo la Mgodi wa Dhahabu wa Kahungwa Majimoto Mining na kusikiliza malalamiko ya wananchi kuhusiana na mgogoro huo, Mhe. Mtambi amesema kuwa timu hiyo itakayowahusisha viongozi, watendaji na walalamikaji itasaidia katika kuweka sawa baadhi ya taarifa zilizopo kabla ya kutoa maamuzi.
“Ninatoa wiki tatu kwa kamati hiyo kukamilisha kazi yake na kuwasilisha taarifa katika ofisi yangu ili niweze kufanya maamuzi kuhusiana na mgogoro huu” amesema Mhe. Mtambi na kuongeza kuwa Mkoa utafanya maamuzi na kuchukua hatua stahiki baada ya kupokea taarifa ya kamati hiyo.
Mhe. Mtambi amesema kamati hiyo itakuwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Afisa Madini Mkoa wa Mara, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na wawakilishi wa walalamikaji na mwekezaji katika mgogoro huo.
Hata hivyo, Mhe. Mtambi amewatahadharisha wananchi wanaotoa taarifa za uongo katika kukuza mgogoro huo na wananchi wanaoleta usumbufu usio na sababu kwa wawekezaji kwa kuwa Mkoa wa Mara utahakikisha wawekezaji katika Mkoa huo wanafanya kazi katika mazingira rafiki ya uwekezaji.
“Mkoa wa Mara hatutamvumilia mtu yoyote anayewavuruga wawekezaji kwa maslahi yake binafsi, tutachukua hatua kali kwa wale wote wanaochochea migogoro isiyo na misingi na wawekezaji” amesema Mhe. Mtambi.
Kwa upande wake akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Serengeti Mhe. Dkt. Amsabi Mrimi amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufika katika eneo hilo kuwasikiliza wananchi na kuunda kamati ya kushughulikia mgogoro huo.
Dkt. Mrimi amewapongeza wananchi wa eneo hilo kwa ustahimilivu katika mgogoro huo na kuwataka kuendelea hivyo ili suluhu yenye manufaa kwa mwekezaji na wananchi iweze kupatikana kwa kufuata sheria za nchi.
Mhe. Mrimi amewataka wananchi wa Majimoto kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo na hususan kutoa taarifa sahihi ili kamati iweze kutekeleza majukumu yake kiufanisi na kupata muafaka wa mgogoro huo mapema iwezekanavyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa