Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ametoa wiki nane kwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kukamilisha nyumba ya mtumishi wa afya iliyojengwa katika Zahanati ya Getarungu kwa nguvu za wananchi ili watumishi wa zahanati hiyo waishi jirani na zahanati hiyo.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kuhusu Halmashauri kutokutekeleza agizo lililotolewa mapema mwaka huu na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara wakati huo Mhe. Said Mohammed Mtanda alipofanya ziara katika zahanati hiyo Machi, 2024.
“Ninataka ndani ya hizo wiki nane nyumba hii iwe inatumika, haiwezekani tumejengewa zahanati nzuri namna hii na Halmashauri inashindwa kukamilisha nyumba iliyojengwa kwa nguvu za wananchi” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Seregeti kusimamia agizo hilo na kuhakikisha Mganga wa Kituo hicho anaishi hapo katika muda huo ili wananchi waweze kupata huduma na hususan wakati wa usiku na kuwaahidi wananchi kuwa baada ya wiki nane ataenda kukagua.
Mhe. Mtambi amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Getarungu kwa kujitolea kujenga nyumba hiyo kwa ajili ya mtumishi wa afya ili waweze kupata huduma za afya.
Aidha, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 na kuhakikisha wanachagua viongozi bora.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Boniface Simbachawene amewataka wananchi kuitunza Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) ili waendelee kupata miradi ya maendeleo kutoka kwa wafadhili.
Akizungumza baada ya kuzindua zahanati hiyo, Mhe Simbachawene amesema zahanati hiyo ambayo ni sehemu ya zahanati nane zilizojengwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) kwa gaharama ya shilingi milioni 387 kila mmoja.
“Manufa haya tunayapata kwa sasa watu wa Getarungu ni wahifadhi wazuri na ndio maana mmefanikiwa kupata mradi huu mkubwa wa zahanati” amesema Mhe. Simbachawene.
Mhe. Simbachawene ameipongeza TANAPA na KFW kwa usimamizi mzuri wa mradi huo, gharama ya mradi inaonekana kupitia mradi huo.
Aidha, Mhe. Simbachawene amewaahidi wananchi kujenga daraja linalounganisha vitongoji wa kijiji hicho ili kuwawezesha wananchi kupata mawasiliano wakati wote na hususan wakati wa masika ambapo mto unaotenganisha vitongoji hivyo ukijaa wananchi wanashindwa kuvuka.
Akiwa katika Wilaya ya Serengeti pia Mhe. Simbachawene ameweka jiwe la msingi katika mradi wa barabara mpya ya stendi mpya- Koreri katika Mji wa Mugumu yenye kilomita nane na madaraja 10 na mitaro yenye thamani ya shilingi milioni 499 inayosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA)
Akizungumza katika eneo hilo, Mhe. Simbachawene ameipongeza TARURA katika utekelezaji mzuri wa mradi huo na kusema kuwa baada ya kukagua na kupokea taarifa ya mradi huo ameiona thamani ya fedha iliyotumika kwenye barabara hiyo.
Ziara hiyo imehudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Mhe. Patrick Chandi Marwa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Serengeti, viongozi wa Halmashauri na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Ziara ya Mhe. Simbachawene imehitimishwa katika Wilaya ya Bunda baada ya kukagua miradi na kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la stendi ya zamani tarehe 4 Oktoba, 2024.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa