Mkuu wa Mkoa leo amefanya ziara katika Halmashauri ya Rorya na kuzungumza na wafanyakazi wa Halmashauri hiyo ambapo ametoa siku saba kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kumrejesha Bwana Fred Kijalawa Afisa Ardhi Mteule aliyehamishiwa Wilaya ya Serengeti kujibu hoja Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo baada ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kumuomba Mkuu wa Mkoa kuwasaidia kumrejesha Bwana Kijalawa ili aisaidie Halmashauri kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusiana na fedha hizo.
“DAS wasiliana na RAS mhakikishe huyu jamaa anarudi na anajibu hoja zote za ukaguzi kuhusiana na mradi huo ambao uliletewa fedha na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ndani ya siku saba” amesema Mhe. Mtambi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mhe. Gerald Ng’ong’a ameeleza kuwa Halmashauri hiyo haipati ushirikiano wanaohitaji kutoka Idara ya Ardhi Wilaya ya Rorya ambayo imekuwa ikitekeleza miradi lakini haitoi taarifa kwenye Baraza la Madiwani.
Mhe. Ng’ong’a ameeleza kuwa Idara hiyo ilipewa fedha za mkopo shilingi bilioni moja ambapo mpaka sasa hamna taarifa ya matumizi ya fedha hizo na kuna hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambazo hazina majibu kutokana na kukosa taarifa.
“Kwa niaba ya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Rorya tunaomba utusaidie kwa kumrejesha Afisa Ardhi aliyehusika na matumizi ya fedha hizo ambaye baada ya hapo alihamishiwa Wilaa ya Serengeti na hatoi ushirikiano katika kujibu hoja tulizonazo” amesema Mhe. Ng’ong’a.
Mhe. Ng’ong’a ameeleza kuwa waliwahi kumuomba KamishnaMsaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mara kusaidia kujibu hoja hizo lakini mpaka sasa hoja zipo na Halmashauri haina majibu ya kuridhisha kuhusiana na matumizi ya fedha hizo katika utekelezaji wa mradi huo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, kwa sasa Idara hiyo imepewa miradi mingine miwili na Baraza la Madiwani halijui gharama za mradi, wanufaika wa mradi, mradi utatekelezwa eneo gani na unamanufaa gani na kumekuwa hakuna ushirikishwaji katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Sisi kama Halmashauri tunataka tupate taarifa ya miradi yote ambayo inatekelezwa na Wizara au taasisi nyingine za umma katika Halmashauri yetu ili tuweze kuijua na kuisimamia miradi hiyo kwa manufaa ya wananchi” amesema Mhe. Ng’ong’a.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mhe. Juma Chikoka ameeleza kuwa Wilaya inaendelea kuwahamasisha wananchi kutunza mifugo yao kwa kujenga mazizi ya pamoja ili kudhibiti wizi wa mifugo katika Wilaya hiyo.
Mhe. Chikoka amewataka wananchi kuipa hadhi inayostahili mifugo yao ili kudhibiti wimbi wa wizi wa mifugo katika wilaya hiyo.
Mhe. Chikoka ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya imeanza kukawakaribisha uwekezaji katika ufuvi na ufugaji wa samaki wa kisasa kwa njia ya visimba na kuongeza kuwa kwa sasa kuna visimba 72 vya wadau na vya Serikali katika Halmashauri hiyo.
Mhe. Chikoka amesema kwa sasa Serikali inatekeleza Mradi wa Maji wa Rorya-Tarime ambapo serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 134 katika mradi huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa