Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo amewapokea na kuzungumza na Maafisa kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) waliopo katika ziara ya kikazi Mkoa wa Mara na kuwataka kuwahamasisha wawekezaji zaidi kuwekeza katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza na maafisa hao, Mhe. Mtambi amesema Mkoa wa Mara una fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo madini, uvuvi, ufugaji na utalii na kuitaka TIC kuwaleta wawekezaji zaidi katika maeneo hayo ili kuchangamkia fursa zilizopo.
“Mkoa wa Mara una malighafi na mazao mbalimbali hata hivyo hauna viwanda vya kutosha kuchakata alighafi hizo kuwa bidhaa na hivyo Mkoa unakosa faida za kiuchumi zinazotokana na malighafi hizo kuchakatwa ili uongezwa thamani” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema kwa sasa mazingira yanaruhusu kwa uwekezaji na miundombinu imeboreshwa kwa ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma.
Mhe. Mtambi amesema Mkoa wa Mara umebarikiwa kuwa na zaidi ya asilimia 70 ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ziwa Victoria na madini katika kila Wilaya ya Mkoa wa Mara lakini fursa hizi bado zinahitaji uwekezaji zaidi ili nchi iweze kupata manufaa makubwa ya kiuchumi.
Kanali Mtambi amewahamasisha wawekezaji mbalimbali kuwekeza katika Mkoa wa Mara na kuwaahidi kuwa kwa kufanya hivyo uwekezaji huo utawalipa mara dufu kwa kuna mahitaji makubwa ya wawekezji kutokana na fursa za uwekezaji zilizopo.
Ameyataja maeneo yaliyobainishwa kwa ajili ya uwekezaji kuwa ni pamoja na Bonde ya Bugwema lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Bonde la Mto Mara ambayo yanafaa kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Kwa upande wake, Meneja wa TIC Kanda ya Ziwa Bi. Fina Jerome amesema Kituo cha Uwekezaji Tanzania kipo katika awamu ya pili ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani kwa kutumia fursa zilizopo nchini.
“Kwa awamu ya kwanza tumeshafika mikoa 17, kwa hii awamu ya pili tunataka kutembelea mikoa iliyosalia kuhamasisha fursa zilizopo katika mikoa hiyo ili zitumike kuinua uchumi wa mikoa hiyo na Taifa kwa ujumla” amesema Bi. Jerome.
Bi. Jerome amesema kupitia kampeni hiyo, TIC inalengo pia la kuangalia changamoto na mazingira ya uwekezaji kwa wawekezaji waliopo ili kutafuta namna ya kuzitatua ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi.
Maafisa wa TIC wapo katika Mkoa wa Mara kwa ajili ya kampeni ya uwekezaji wa ndani awamu ya pili ambapo kesho tarehe 23 Julai, 2024 maafisa hao wataendesha semina ya kwanza ya uwekezaji kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara katika ukumbi wa uwekezaji.
Kwa leo, mbali na kuwasili Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na kutia saini kitabu cha wageni, Maafisa hao wametembelea Wilaya ya Tarime kujionea uzalishaji katika baadhi ya viwanda na migodi ya kati iliyopo katika Wilaya hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa