Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo amezungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na kuitaka Halmashauri hiyo kuongeza uwekezaji katika Ziwa Victoria ili kupanua wigo wa mapato ya Halmashauri hiyo yanayotokana na kuwepo kwa sehemu kubwa ya Ziwa Victoria.
Mhe. Mtambi ameeleza kuwa kwa sasa Halmashauri hiyo inapata mapato yanayotokana na shughuli za uvuvi wa samaki tu na kuitaka Halmashauri kusafisha fukwe za Ziwa Victoria na kuvutia wawekezaji katika ugufaji wa kisasa wa samaki, uwekezaji kwenye fukwe, shughuli za usafirishaji katika Ziwa Victoria na ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki, nyama na mazao.
“Kukiwa na boti za kisasa na usafiri mzuri katika Ziwa Victoria itakuwa rahisi kwa watalii baada ya kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kutalii pia katika Ziwa Victoria jambo ambalo litakuza uchumi wa Mkoa na mwananchi mmoja mmoja” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi ameeleza kuwa usafiri mzuri katika Ziwa Victoria utapanua uwekezaji wa hoteli za kisasa kandokando ya ziwa na kuongeza ajira kwa wananchi wa Wilaya ya Rorya na kuimarisha masoko ya wakulima, wafugaji na wavuvi baada ya watalii kuongezeka.
Mhe. Mtambi ameeleza kuwa Wilaya hiyo ina eneo lenye mita za mraba 9,345 ambapo asilimia 77 ya eneo hilo ni Ziwa Victoria wakati Halmashauri inapata mapato kidogo yanayotokana na Ziwa Victoria kwa sababu hamna uwekezaji uliofanyika katika Ziwa na fukwe za Ziwa hilo .
“Tuweke mipango na mikakati inayoendana na jiografia ya eneo la Wilaya ya Rorya ili tutumie vizuri jiongrafia hiyo kupanua vyanzo vya mapato ili kupata maendeleo endelevu ya Wilaya ya Rorya” Amesema Mhe. Mtambi.
Wakati huo huo, Mhe. Mtambi ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kwa kufanikiwa kukusanya shilingi 1,535,618,289 hadi kufikia tarehe 27 Mei, 2024 ambayo ni sawa na asilimia 97 ya makusanyo ya mapato ya ndani yaliyopangwa kukusanya ya shilingi 1,590,456,000 katika mwaka wa fedha 2023/2024.
“Baada ya kufanya uwekezaji katika Ziwa Victoria mapato ya wilaya hii yatakuwa endelevu kutokana na kuongezeka kwa biashara za mpakani kati ya Tanzania, Kenya na Uganda pindi usafiri wa majini ukiwa umeimarika” amesema Mhe. Mtambi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mhe. Gerald Ng’ong’a ameeleza kuwa Baraza la Madiwani linaendelea kuisimamia Halmashauri na kufanikisha kupandisha makusanyo ya mapato ambapo hadi tarehe 27 Mei, 2024 Halmashauri imefanikiwa kukusanya shilingi 1,535,618,289.
Mhe. Ng’ong’a ameeleza kuwa Halmashauri katika mwaka wa fedha 2023/2024 ilipanga kukusanya shilingi 1,590,456,000 ambapo makusanyo mpaka sasa ni sawa na asilimia 97 ya makusanyo yote ya mwaka huu.
Mhe. Ng’ong’a ameeleza kuwa Halmashauri hiyo inategemea kuongeza zaidi mapato ya ndani baada ya kuwekeza katika ujenzi wa stendi katika eneo la Mika na matarajio stendi hiyo ikianza kutumika mapato yataongezeka.
Mwenyekiti huyo wa Halmashauri amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Madiwani na wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya jambo ambalo amesema linafanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi pamoja na Halmashauri hiyo kupata hati safi ya ukaguzi kwa miaka mitatu mfululizo.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rorya Bwana Michael Bundala amewapongeza wafanyakazi kwa kazi nzuri wanazozifanya na kuiwezesha Halmashauri kupata hati safi ya ukaguzi.
Mhe. Bundala ameipongeza Halmashauri kuhusu ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuitaka Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kukumbuka kurejesha asilimia ya makusanyo yake kutekeleza miradi ya maendeleo katika vijiji.
Mhe. Bundala amewataka wataalamu wa Halmashauri kuwaandaa wananchi wa Wilaya ya Rorya kuchangamkia fursa za miikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya vikundi vya akina mama, watu wenye ulemavu na vijana itakapoanza kutolewa Julai, 2024.
Mhe. Bundala amewataka viongozi na wataalamu wa Wilaya ya Rorya kutimiza wajibu wao na kuwahudumia wananchi na kutatua kero zao.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa