Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amekabidhi Kompyuta 142 kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya mawasiliano katika Zahanati, amewataka wasimamizi wa Sekta ya Afya kuhakikisha matumizi ya Mfumo wa GOTHOMIS unafika asilimia 100 katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika Hafla hiyo, Mhe. Mtambi amesema awali, Mkoa wa Mara ulikuwa unashika nafasi ya kwanza katika ufungaji na matumizi ya mfumo huo katika vituo vya kutolea huduma za afya na kwa sasa umeshuka baada ya mikoa mingine kuongeza jitihada.
“Sasa mhakikishe tunarudi kwenye nafasi yetu ya awali, na hii inawezekana baada ya kupata msaada huu ambao unaenda kutatua changamoto ya ukosekanaji wa vifaa katika vituo vya kutolea huduma za afya” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema kwa sasa Mkoa hauna sababu ya kuendelea kubaki na matumizi ya mfumo wa GOTHOMIS kwa asilimia 90 na kuitaka Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kuhakikisha kuwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinafunga na kutumia mfumo huo.
Aidha, Mhe. Mtambi ametoa hadi tarehe 30 Agosti, 2025 vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara viwe vimefungwa mfumo wa GOTHOMIS na kuzitaka Divisheni za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii vya Halmashauri kusimamia matumizi sahihi ya vifaa vilivyotolewa.
Kanali Mtambi amekemea tabia ya watumishi wa sekta ya afya kuchelewesha kutoa huduma kwa wananchi kwa kisingizio kuwa mfumo unasumbua ili watoe huduma nje ya mfumo jambo ambalo amesema linasababisha wizi wa fedha za Serikali.
“Watumishi ambao hawaujui vizuri mfumo au matumizi ya kompyuta wajifunze na kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuboresha utendaji wao na kutoa huduma bora kwa wananchi bila visingizio” amesema Mhe. Mtambi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya amesema vifaa hivyo vitausaidia Mkoa wa Mara katika kuimarisha matumizi ya mfumo wa GOTHOMIS ambao unaenda kudhibiti mapato ya Serikali katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Aidha, Ndugu Kusaya amesema matumizi ya mfumo yakiimarisha yatawezesha pia mawasiliano kuboreshwa kati ya vituo vya kutolea huduma za afya na taasisi mbalimbali za Serikali.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu ameishukuru Wizara ya Afya kwa kutoa Kompyuta hizo kwa Mkoa wa Mara na kuahidi kuzitumia kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.
“Vifaa hivi vitasaidia kuboresha upatikanaji wa vifaa katika matumizi ya mifumo mbalimbali ya afya ili kutuwezesha kudhibiti mapato ya Serikali na utoaji wa taarifa kwa wakati” amesema Dkt. Masatu.
Halfa hiyo imehudhuriwa na Wakuu wa Sehemu na Vitengo vya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Kaimu Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Mara, Wakuu wa Divisheni za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa