MTAMBI ATAKA MABADILIKO KUTOKA KWA WAVUVI
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amefanya kikao na wavuvi wa Mkoa wa Mara katika ukumbi wa uwekezaji na kuwataka viongozi wa vyama vya uvuvi katika Mkoa wa Mara kuwaongoza wavuvi na kuleta mabadiliko chanya kwa wanachama wao.
Mhe. Mtambi amesema hayo wakati wa kuhitimisha kikao hicho na kuwataka makundi yote ya wavuvi kuungana na kuchagua uongozi wa wavuvi ukijumuisha viongozi wa makundi yote ndani ya siku saba ili kuimarisha Umoja wa Wavuvi wa Mkoa wa Mara.
“Ukiwa kiongozi unatakiwa kuonyesha mfano na kuonyesha njia ya kufikia maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili kama wavuvi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo” amesema Mhe. Mtambi.
Amewataka viongozi wa wavuvi kuanzisha operesheni ya kudhibiti uvuvi haramu katika maeneo yao na kuwasimamia wavuvi waliochini yao ili waweze kuvua kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi na kuacha kulindana wao kwa wao wanapokuwa wamekiuka sheria na taratibu.
Mhe. Mtambi amewataka viongozi na wavuvi kutoa taarifa pale wanapohisi wanakwama au wanakwamishwa kutekeleza majukumu yao au wanapowabaini wavuvi haramu ambao wanashindwa kuwadhibiti katika maeneo yao.
Mhe. Mtambi amewataka vongozi na watendaji wa Serikali kuhakikisha kuwa Kamati za Usimamizi za Rasilimali za Uvuvi (BMU) zinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni na kuwataka wanasiasa kuacha kuingilia utendaji wa kamati hizo katika maeneo yao.
Mhe. Mtambi amesema eneo la Mkoa wa Mara asilimia 36 ni Ziwa Victoria lakini mapato yanayotokana na Ziwa hilo yanahusisha uvuvi peke yake na kwa kiasi kikubwa Mkoa haufaidi eneo hilo kutokana na uvuvi haramu unaoendelea kwa kiasi kikubwa.
Mhe. Mtambi ameagiza kuteketezwa kwa nyavu zote zilizokamatwa zilizopo katika bohari siku ya Ijumaa tarehe 19 Julai, 2024 na kuwataka viongozi wa vyama vya wavuvi kusaidia kuteketeza nyavu haramu wanazokamata katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa Bwana Gerald Musabila Kusaya amesema Mkoa wa Mara una eneo lenye kilomita za mraba 10,854 za maji ya Ziwa Victoria ambayo ni sawa na asilimia 36 ya eneo lote.
Bwana Kusaya amesema Mkoa una mialo ya uvuvi 151 na kati ya hiyo 127 ni mialo rasmi huku mialo 24 ikiwa sio rasmi lakini inatumiwa na wavuvi wa Mkoa wa Mara wapatao 17,093 wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Victoria na Mto Mara.
Bwana Kusaya amesema, Mkoa wa Mara una wavuvi wengi na watu ambao wanahusika na mnyororo wa uvuvi ikiwemo wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi ambao ni wengi na wote maisha yao yanategemea kukua kwa sekta ya uvuvi.
Amesema kwa sasa Serikali imeboresha mazingira katika sekta ya uvuvi ikiwemo na utoaji wa mikopo ya wavuvi na wafugaji wa samaki kwa riba nafuu kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ambapo tayari baadhi ya wavuvi wa Mkoa wa Mara wamenufaika na mikopo hiyo.
Kwa upande wake,mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Omari Gamuya amesema katika maeneo ya wavuvi kuna takriban kaya 96,097 ambazo hazina vyoo bora na kuwahamasisha wavuvi kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo yao na mialo ya uvuvi ili kupunguza uwezekano wa kutokea kwa magonjwaya mlipuko.
Dkt. Gamuya amesema katika mialo, kambi za wavuvi na maeneo yao ya makazi kwa sehemu kubwa hayana vyoo bora na hivyo wengi wao hawatumii vyoo katika kujisaidia jambo ambalo ni hatarishi kwa maisha ya watu katika maeneo hayo.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wakurugenzi wa Halmashauri na Wataalamu wa Uvuvi kutoka Halmashauri saba za Mkoa wa Mara zinazojihusisha na uvuvi ambazo ni Musoma Manispaa, Musoma DC, Bunda DC, Butiama DC, Bunda TC, Rorya na Tarime DC.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa