Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amewapokea na kuzungumza na wanachama wa Mgodi wa IRASANILO unaomilikiwa na wachimbaji wadogo katika eneo la Buhemba, Wilaya ya Butiama na kutaka mabadiliko katika uendeshaji wa kikundi hicho.
Mhe. Mtambi amesema mgodi huo una mapato makubwa lakini bila kufanya mabadiliko ya namna ya uendeshaji wa kikundi hicho na kuweka nidhamu katika matumizi ya fedha za kikundi hicho, mgodi huo utaendelea kuwa na jina kubwa na mapato makubwa lakini wanakikundi hawatapata manufaa yoyote.
“Kikundi chenu mngetulia vizuri kingekuwa na matajiri wakubwa sana katika Mkoa wa Mara na mngeweza kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali ambao ungewaza kuyabadilisha mambo katika Mkoa wa Mara na maisha yenu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema ili kukisaidia kikundi cha IRASANILO maafisa wa Serikali wataisoma katiba ya kikundi hicho na kuifanyia marekebisho katika mapungufu watakayoyaona na kulingana na maoni waliyotoa leo, wakikubaliana watafanya uchaguzi Mkuu ili waweze kupata viongozi wapya wa kikundi hicho.
Mhe. Mtambi amesitisha zoezi la uchaguzi wa viongozi wa mgodi huo lililokuwa linalalamikiwa na wanachama wake mpaka hapo katiba na kanuni za kikundi hicho zitakapotiwa na kukubalika upya na wanachama wote wa mgodi huo.
Aidha, ameitaka IRASANILO kuangalia uwezekano wa kubadilisha katiba na kumweka Mkuu wa Mkoa wa Mara kuwa mlezi wa kikundi hicho ili awasaidie kukisimamia kwa karibu na kupata taarifa zote za uendeshaji wa kikundi hicho kwa kufuata sheria, miuongozo na taratibu za vikundi vinavyohusika na madini.
Mhe. Mtambi ameeleza kuwa awali amepokea malalamiko kutoka kwa wanachama wa mgodi wa IRASANILO wakilalamikia kuhusiana na mchakato wa uchaguzi uliofanyika mara ya mwisho, wizi wa fedha za kikundi na ukiukwaji wa katiba ya kikundi hicho katika uendeshaji wa kikundi hicho.
Mhe. Mtambi ameagiza Kamishna Msaidizi wa Madini Mkoa wa Mara kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi uliokuwa unaendelea katika kikundi hicho usimame kupisha marekebisho ya katiba na kanuni za uendeshaji wa mgodi huo zipitiwe upya kusadifu mahitaji ya sasa ya kikundi hicho.
Mhe. Mtambi ameagiza Kamati ya Migogoro ya Mkoa wa Mara hadi kufikia Ijumaa ya tarehe 15 Novemba, 2024 iwe imekutana na wachimbaji wadogo na kuwahusisha wadau mbalimbali kupitia katiba yao ya sasa ili kutoa maoni na kuwasilisha rasimu ya katiba mpya ambayo itajadiliwa na kupitishwa na wanachama wote.
Mhe. Mtambi ameahidi baada ya uchaguzi na viongozi wapya kupatikana, Mkoa utafanya ukaguzi ili kujiridhisha na uendeshaji wa Mgodi wa IRASANILO na kukagua ukaguzi uliofanywa awali na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na kutoa matokeo ya ukaguzi ndani ya muda mfupi.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Mgodi wa IRASANILO Bwana Shaban Omari Wambura ameeleza kuwa matatizo mengi yanatokana na wanachama wengi hawafanyikazi katika mashimo waliyonayo na wanataka fedha za bure kutoka kwa viongozi wa IRASANILO.
Zamani ilikuwa wanalipia asilimia 18 kwa sasa ni asilimia 08. Viongozi wa sasa wanafanya kazi wao wenyewe. Roho za kutofanya kazi na kutaka kuwanyonya wengine. Kwa sasa kimekuwa ni kijiwe cha majungu na wengi hawafanyi kazi.
Kwa upande wake, Hassan Kinyenga mwanachama wa IRASANILO ameeleza kuwa tatizo la chama hicho ni msingi walioanza nao kama chama na wamekuwa na makundi mengi kwa msingi wa ukabila, udini na kipato na kufanya ubaguzi kwa watu wengine ambao hawamo kwenye kundi lake.
Bwana Kinyenga ameeleza kuwa hakuna kiongozi wanayemchagua anamaliza muda wake wa uongozi, viongozi wengi wanaondolewa na vikundi vya watu wachache kutokana na sababu za ukabila, udini na kipato chao.
Bwana Kinyenga ameeleza kuwa ili kuwaondoa viongozi, wanakikundi wanajigawa kwa namna ya ukabila, udini na uwezo wa watu na wanaundiwa tuhuma mbalimbali wanaondolewa na wakati mwingine wahusika wanaowaondoa viongozi sio wanachama bali ni watu nje ya chama wanaochochea wanachama kufanya mabadiliko.
Bwana Kiyenga ameeleza kuwa awali alikuwa mjumbe wa Kamati Tendaji nay eye pamoja na viongozi wenzake waligundua milioni 150 zimeibiwa na viongozi wakaundiwa zengwe na kuondolewa kwenye uongozi wa kikundi hicho.
Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Mara (MALEMA) Bwana David Mwita, ameeleza kuwa wachimbaji wadogo wa IRASANILO wanayo matatizo makubwa na wanamshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutenga muda wake na kuwasikiliza wachimbaji hao na kuwatafutia ufumbuzi.
Bwana Mwita amemuomba Mkuu wa Mkoa katika marekebisho ya katiba ya IRASANILO ziangaliwe pia na kanuni zinazotumika katika uendeshaji wa kikundi hicho kwani anahisi kanuni hizo pia zinatoa baadhi ya mianya inayotumika na wasioutakia mema mgodi huo.
Bwana Mwita amesema viongozi waliopo madarakani kwa sasa kuna vitu wamefungwa hawatakiwi kuvifanya kutokana na barua waliyopewa na Serikali ya kuwazuia viongozi hao wa mpito kuvifanya ikiwa ni pamoja na kufanya uchaguzi wa viongozi wake.
Ameeleza kuwa uongozi wa MALEMA Wilaya na Mkoa hawakuhusishwa katika kufanya vetting ya wagombea katika uchaguzi wa mgodi wa IRASANILO na kuongeza kuwa ukaguzi wa hujuma za kifedha IRASANILO uliokuwa unafanyika umefanyika kwa gharama kubwa na haukufanyika kama inavyotakiwa.
Bwana Mwita amevitaka vyama vinapokuwa na migogoro kuwasilisha migogoro yao kwa uongozi wa MALEMA na migogoro hiyo ikishafika Serikalini MALEMA haina nafasi ya kuishughulikia tena baada ya kupokelewa na viongozi wa Serikali.
Aidha amewataka wachimbaji kufunguka katika uwekezaji wao na sio lazima kufanya uchimbaji katika sehemu moja na kuwataka watafute leseni za maeneo mbalimbali ili waweze kutanuka kiuchumi na kimawazo.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ofisi ya Afisa Madini Mkoa wa Mara na wajumbe wa Kamati ya Mgogoro ya Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa