Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ametembelea ujenzi wa Chuo cha Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) katika eneo la Burunga, Kata ya Uwanja wa Ndege na kutaka kasi ya ujenzi wa chuo hicho iongezeke ili ujenzi uweze kukamilika haraka.
Mhe. Mtambi pia amemtaka Mhandisi anayesimami mradi huo kuwepo eneo la mradi atakapokuja kukagua tena baada ya siku 14 ili atoe taarifa ya kitaalamu kwa nini mradi huo umechelewa kukamilika kinyume na maelekezo ya Serikali.
“Mimi nitakuja hapa baada ya siku 14 kuona maendeleo ya ujenzi, ninataka kuona mabadilko na majibu ya vifaa vinavyotakiwa kuletwa katika eneo la ujenzi na Wizara (Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia) ili tupate hatma ya ukamilishaji wa mradi huu” amesema Mhe. Mtambi.
Kwa upande wake, Mthibiti Ubora wa Wilaya ya Serengeti Bwana Nyoyo Andrea Nyangati ambaye ndio msimamizi wa mradi huo kwa niaba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema ujenzi huo ni awamu ya kwanza ya mradi huo na inahusisha majengo tisa (9) kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni moja.
Bwana Nyangati ameeleza kuwa kwa sasa ujenzi wa majengo hayo umefikia asilimia 47 na baadhi ya majengo ujenzi wake umesimama wakisubiria vifaa kutoka kwa wazabuni waliopewa zabuni na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Bwana Nyangati ameeleza kuwa mpaka sasa ujenzi huo umepokea jumla ya shilingi 345,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa maboma yote na kupandisha kuta za baadhi ya majengo ya Chuo hicho na majengo mengine kusubiria vifaa vya ujenzi kutoka Wizarani.
Bwana Nyangati ameeleza changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi huo ni pamoja na mvua za vuli na masika zilizokuwa zinanyesha kuzuia upelekaji wa vifaa vya ujenzi katika eneo hilo, uhaba wa maji ambao ulitatuliwa kwa kujenga kisima kilichokusanya maji ya mvua.
Changamoto nyingine ni okosefu wa umeme katika eneo la mradi na kutokuwepo kwa barabara ya uhakika ya kufika katika eneo la mradi wa ujenzi na hivyo kukwamisha upelekaji wa vifaa na hususan wakati wa mvua za vuli na masika.
Chuo cha VETA ni sehemu ya vyuo vya VETA vinne vinavyoendelea kujengwa kwa awamu hii katika Mkoa wa Mara ambapo vingine vinajengwa katika Wilaya za Tarime, Rorya na Bunda huku Serikali ikiwa imekamilisha ujenzi wa Chuo cha VETA Wilaya ya Butiama mwaka 2022.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na baadhi ya Wajumbe wa Kamatiya Usalama ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti, Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mwenyekiti na Menejimenti ya Wilaya ya Serengeti na maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, taasisi na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa