Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameshiriki kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri wa Mji wa Bunda na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kwenda Halmashauri ya Mji wa Bunda kujifunza namna ya kujibu hoja za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Ninatoa muda mfupi Halmashauri zote za Mkoa wa Mara zije kujifunza hapa namna ya kujibu hoja za ukaguzi ili zikaboresha taarifa zao na za utekelezaji wa hoja za ukaguzi na maelekezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)” amesema Mhe. Mtambi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi pia ameipongeza Halmashauri kwa kupata hati safi ya ukaguzi kwa miaka minne mfululizo na kuwa na hoja chache za ukaguzi baada ya kufanikiwa kufunga hoja nyingi zilizokuwa zimehojiwa na CAG hapo awali.
Mhe. Mtambi ameipongeza Halmashauri hiyo kwa makusanyo ya mapato ya ndani ambapo hadi kufikia tarehe 31 Mei, 2024 Halmashauri hiyo ilikuwa imekusanya shilingi 1,879,551,750 kati ya lengo la kukusanya shilingi 2, 058,480,000 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mhe. Mtambi amesema makusanyo hayo ni sawa na asilimia 91.3 ya fedha yote iliyopangwa kukusanywa na kuongeza kuwa ni matumaini yake watafikia malengo ya makusanyo hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2024.
Mhe. Mtambi ameitaka Halmashauri hiyo kuandaa mpango kazi na kusimamia utekelezaji wa kujibu hoja za ukaguzi na maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) kwa wakati.
Mhe. Mtambi ameitaka Halmashauri kutumia Mfumo wa Taifa wa Manunuzi (NEST) katika kufanya manunuzi na kufanya mafunzo kwa watumishi na Madiwani kuhusu mfumo wa NEST, sheria ya manunuzi ya mwaka 2023 na kanuni zake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bunda Mhe.Mayaya Abraham Magese amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kazi nzuri anayoifanya tangu alipoingia Mkoa wa Mara na hususan katika ukaguzi wa miradi ya maendeleo na ufuatiliaji wa utendaji wa watumishi.
Amemshukuru Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Mhe. Michael Kweka na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kusimamia Halmashauri hiyo katika utendaji wake.
Mheshimiwa Magese ametolea mfano wa hoja za CAG ambapo Halmashauri hiyo katika ukaguzi wa mwaka 2022/2023 ilipata hoja 21 na hadi sasa imefanikiwa kufuta hoja 13 na sasa imebakiza hoja nane tu na sehemu kubwa ya hizi hoja zipo nje ya uwezo wao.
Mheshimiwa Magese amesema huwa Halmashauri hii wanafanya kazi vizuri na Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Bunda hakina wasiwasi na usimamizi wao wa miradi na utoaji wa huduma kwa wnaanchi.
Katika ukaguzi wa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Mji wa Bunda ulipata hoja 21 na kati ya hoja hizo, hoja 13 zimehakikiwa na kufungwa na kwa sasa bado hoja 8 ambazo zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Aidha, Halmashauri hiyo ilikuwa na hoja za miaka ya nyuma 38 na kati ya hoja hizo, hoja 24 zilihakikiwa na kufungwa, hoja 11 zipo kwenye hatua za utekelezaji, hoja 2 zimejirudia na hoja 1 imepitwa na wakati.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa