Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi katika utaratibu wake wa kawaida wa kusikiliza kero za wananchi siku ya Ijumaa, leo tarehe 5 Julai, 2024 amesekiliza kero za wananchi katika ukumbi wa uwekezaji Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na kutoa maamuzi mbalimbali.
Mhe. Mtambi amemsikiliza Bibi Joyce Marwa Matiku (66) ambaye nyumba yake pamoja na shamba viliuzwa mwaka 2017 na mtoto wake wa kwanza Joseph Marwa Matiku (49) na kesi imeenda hadi mahakama kuu lakini haikuwa inapata maamuzi kutokana na makosa ya ufunguaji wa kesi kwa sababu hakuwa na wanasheria wa kumsimamia.
Katika maamuzi yake, Mhe. Mtambi amempatia mawakili watakaomsaidia kufungua upya kesi hiyo na kumueleza Bibi Matiku kuendelea kuishi katika nyumba hiyo iliyouzwa mpaka maamuzi ya Mahakama yatakavyotolewa baada ya kuwa amesimamiwa na mawakili aliompatia yatakapoamuru vinginevyo.
Mhe. Mtambi amewasilikiza wananchi wa Kijiji cha Bumangi, Wilaya ya Butiama ambao eneo lao walilopanga kujenga soko liligawiwa kwa makosa na dalali wa mahakama katika kesi ya talaka baina ya wanandoa wawili na eneo hilo kupewa mke wa wanandoa hao.
Katika maamuzi yake, Mhe. Mtambi amewataka viongozi hao kuendelea kulitumia eneo lao lililogawiwa katika kesi ya talaka ya wanandoa hao na kama kuna mtu atakuja kuwaondoa wawataarifu viongozi wa Wilaya ya Butiama na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Kanali Mtambi amewasikiliza wananchi wanaoidai fidia Manispaa ya Musoma baada ya maeneo yao kutumika kujenga shule za Sekondari za kata na kuwataka kufika jumatatu tarehe 8 Julai, 2024 wakiwa na vielelezo vyao ambapo pia Mkurugenzi na baadhi ya maafisa kutoka Manispaa ya Musoma wataitwa kujibu hoja zao.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ametoa kibali kwa mwananchi aliyekuwa na shamba katika eneo lililouzwa kwa Wakala wa Vipimo kwenda kukata miti yake iliyokuwa katika eneo hilo kabla halijauzwa kwa Wakala wa Vipimo.
Katika kusikiliza kero za wananchi, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Bwana Dominicus Lusasi, Kamati ya kusikiliza Kero za wananchi aliyoiunda na baadhi ya Maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa