Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amefunga kikao cha mwaka cha Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) na kuwapongeza walimu waliofanikisha ufaulu wa wanafunzi wa Kidato cha Sita mwaka 2023 katika matokeo ya mtihani wa Taifa.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho, amesema ni matumaini ya viongozi wa Mkoa wa Mara kuwa matokeo yale yatakuwa endelevu na yatafikiwa pia kwa wanafunzi wa Kidato cha Pili na cha Nne kama wataongeza juhudi katika usimamizi ufundishaji na ujifunzaji.
“Katika matokeo ya Kidato cha Sita Mkoa ulifaulisha kwa asilimia 100 na katika Mkoa mzima kulikuwa hamna ufaulu wa daraja la nne na sifuri na kuuwezesha mkoa kushika nafasi nzuri kitaifa” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi amewataka Wakuu wa Shule kuongeza jitihada na kuwawezesha wanafunzi kufaulu mitihani yao hususan kwa Kidato cha Pili na cha Nne ambapo amesema Mkoa wa Mara haufanyi vizuri sana katika mitihani ya Taifa kutokana na sababu mbalimbali.
Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Shule kusimamia walimu na wanafunzi na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao katika mazingira ya shule na kudhibiti utoro wa rejareja wa wanafunzi kwa kuwahusisha viongozi, wazazi na walezi wa wanafunzi hao.
Kanali Mtambi amewataka Wakuu wa Shule kusimamia nidhamu za walimu na wanafunzi na kuhakikisha Shule zinakuwa mazingira salama kwa wanafunzi kujifunza maadili mema na masomo yao bila ya kuwa na vishawishi kutoka kwa walimu.
Aidha, amewataka Wakuu wa Shule kusimamia utekelezaji wa miradi ya Serikali katika maeneo yao na kwa kuzingatia ubora na maelekezo ya Serikali katika miradi husika na manunuzi yote ya miradi yafanyike kupitia mfumo wa manunuzi ya umma ili kupunguza hoja za ukaguzi.
“Serikali imewekeza sana katika miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu ambapo mwaka 2023/2024 Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 17 kwa ajili ya ujenzi wa miradi katika shule za Msingi na Sekondari katika Mkoa wa Mara” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema Serikali imeboresha na inaendelea kufuatilia maslahi ya walimu kwa kutambua mchango wao katika malezi na ujifunzaji wa watoto katika kuimarisha taaluma na kuwaahidi kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu ili watimize wajibu wao kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAHOSSA Mkoa wa Mara Mwalimu Magudila Mgeta amesema hicho kilikuwa ni kikao cha mwaka cha TAHOSSA na kimejadili mambo mbalimbali ikiwemo kupokea maelekezo kutoka kwa viongozi kuhusiana na uboreshaji wa taaluma.
Bwana Mgeta amesema moja ya agenda iliyojadiliwa kwa muda mrefu ni namna ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi na hususan katika mitihani ya Kidato cha Pili na Kidato cha Nne katika Mkoa wa Mara na kupeana mikakati ya kuboresha ufaulu huo.
Kikao hicho cha siku mbili kimefanyika kuanzia jana na leo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Songe iliyopo Manispaa ya Musoma na kuwakutanisha Wakuu wa Shule za Sekondari 301 za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa