Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ametembelea Shule ya Sekondari Ngoreme, Wilaya ya Serengeti kukagua utekelezaji wa maagizo aliyotoa tarehe 13 Agosti, 2024 kuhusu Halmashauri kukamilisha bweni lililojengwa kwa michango ya wananchi na wadau na kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa hatua iliyofikia katika ukamilishaji wa bweni hilo.
Mhe. Mtambi ametoa pongezi hizo baada ya kukuta mafundi wakiwa wanaendelea na shughuli za ukamilishaji ikiwemo kujenga ngazi kwenye milango ya kuingilia na kupaka rangi awamu ya pili kwa ndani ya jengo hilo ambalo lilikuwa limeachwa bila kukamilishwa kwa miaka saba.
“Ninaipongeza sana Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa hatua iliyofikia katika ukamilishaji wa bweni hili na kuitaka kukamilisha ndani ya wiki sita walizopewa na kuwasilisha taarifa kuhusiana na utekelezaji wa agizo hilo” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi ameitaka Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa baada ya wiki sita alizotoa kukamilika, wanafunzi waliokuwa wanalala katika vyumba vya madarasa wanahamia katika bweni hilo baada ya kukamilika.
Aidha, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kukamilisha uingizaji wa maji na umeme katika bweni hilo ili wanafunzi wakae sehemu salama kwa matumizi yao.
Mhe. Mtambi amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Serengeti kwa usimamizi wake katika utekelezaji wa maagizo hayo na kumtaka kuhakikisha kuwa Halmashauri inakamilisha umaliziaji wa bweni hilo ndani ya muda waliyopewa.
Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya, Halmashauri na taasisi za Serikali kutoa ushirikiano kwa viongozi wa kimila na machifu waliopo katika maeneo yao.
Mhe. Mtambi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Serengeti kuhakikisha wataalamu kutoka SENAPA, TAWA na TFS wanashughulikia tatizo la nyani na gendere katika eneo hilo la Ngoreme kuanzia tarehe 21 Septemba, 2024 ili wananchi waweze kuzalisha chakula katika mashamba yao.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ngoreme Mwalimu Daniel Mgaya amesema ujenzi wa bweni hilo umefanywa na Jumuiya ya Maendeleo Ngoreme na kuwekewa jiwe la msingi na Mwenge wa Uhuru mwaka 2017.
Mwalimu Mgaya amesema baada ya Mkuu wa Mkoa kutoa maelekezo ya kukamilisha ujenzi wa bweni hilo tarehe 13 Agosti, 2024, tarehe 14 Agosti, 2024 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Serengeti alileta wataalamu kwa ajili ya kufanya tathmini ya kazi na gharama inayohitajika na baadaye alileta shilingi milioni 26.6 kwa ajili ya ukamilishaji wa bweni hilo.
Mwalimu Mgaya amesema shughuli zilizofanyika mpaka sasa ni pamoja na kufunga dari, sakafu, kukamilisha madirisha, kupaka rangi ndani na nje na kuongeza kuwa shughuli zinazoendelea kwa sasa ni kupaka rangi kwa mara nyingine kwa ndani na kujenga ngazi katika jengo hilo.
Kwa mujibu wa Bwana Mgaya kazi ambazo hazijakamilishwa ni kutengeneza meza ya kunyooshea nguo na kufulia katika bweni hilo pamoja na kuingiza umeme na maji katika bweni hilo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara aliambatana na Wakuu wa Wilaya za Musoma, Tarime na Serengeti, Diwani wa Kata ya Kenyamonte na wananchi wa eneo hilo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa