Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amekutana na kuzungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bwana Amon Anastaz Mpanju ambaye yupo Mkoani Mara kwa lengo la kuzungumza na wafanyabiashara wadogo wadogo kuhusiana na mikopo mipya kwa wajasiriamali itakayotolewa na Serikali kupitia Benki ya NMB.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi ameipongeza Serikali kwa kuanzisha mikopo kwa ajili ya wajasiriamali na kuongeza kuwa jambo hili limefika wakati muafaka kwa kuwa amekuwa akipokea maombi kutoka kwa wajasiriamali na hususan ambao walikuwa hawapewi mikopo inayotolewa na Halmashauri.
“Ninaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita kuja na wazo hili, kuna kundi kubwa la wananchi ambao walikuwa hawawezi kupata mikopo ya Halmashauri lakini na wao sasa watanufaika na mikopo hii itakayotolewa na Serikali” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema kwa wananchi kupata uhakika wa mikopo yenye riba nafuu, itawasaidia kuanzisha na kuendeleza biashara zao na kuachana na mikopo inayotolewa na taasisi ambazo hazijasajiriwa ambayo inawaumiza wajasiriamali.
Kwa upande wake, Bwana Mpanju amesema mpango wa Serikali kutoa mikopo upo katika hatua nzuri ambapo tayari Benki ya NMB imeshinda kwa ajili ya kutoa mikopo hiyo kwa riba ya asilimia saba isiyoongezeka.
Bwana Mpanju amesema ili kunufaika na mikopo hiyo wajasiriamali wanatakiwa kuwa na vitambulisho vya wajasiriamali ili kuweza kutambulika shughuli wanazofanya na kuweza kunufaika na mikopo hiyo ya wajasiriamali.
Bwana Mpanju amesema vitambulisho vya wajasiriamali vinatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 17 Oktoba, 2024 katika Mkoa wa Arusha wakati utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali unatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba, 2024.
Bwana Mpanju ameeleza kuwa mikopo hii itawasaidia wajasiriamali kukuza mitaji yao kwa sababu haina kikomo cha kukopa kutegemeana na makubaliano yatakayofikiwa kati ya mjasiriamali na Benki ya NMB na wazo la mjasiriamali katika biashara anayotegemea kuifanya.
Bwana Mpanju pia amezungumza na wajasiriamali wa Wilaya ya Musoma katika ukumbi wa uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ambao amewataka viongozi wa wajasiriamali kuwahamasisha wajasiriamali kupata vitambulisho vya wajasiriamali vitakavyowasaidia kupata mikopo hiyo yenye riba nafuu.
Akiwa kwenye mazungumzo hayo, Bwana Mpanju ametolea ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa na wajasiriamali walioshiriki kikao hicho na kuwahamasisha kuwahamasisha wenzao kuchukua kadi za wajasiriamali.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na maafisa kutoka Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa