Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Afred Mtambi leo ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Maadhimisho ya 13 ya Siku ya Mara yanayofanyika kuanzia tarehe 12 Septemba, 2024 hadi tarehe 16 Septemba, 2024 katika Mji wa Sekenani, Narok nchini Kenya.
Mhe. Mtambi na ujumbe wake uliwasili katika Mji wa Narok jana jioni na leo Kanali Mtambi pamoja na viongozi wengine wamepanda miti wa kumbukumbu ya Maadhimisho ya 13 ya Siku ya Mara katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara Mjini Narok na baadae kushiriki katika Kongamano la kisayansi kuhusu uhifadhi wa ikolojia ya bonde la Mto Mara lililofanyika katika ukumbi wa chuo hicho.
Katika maadhimisho haya, Mhe. Mtambi ameambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerard Musabila Kusaya, Wakuu wa Wilaya, Meya na Wenyeviti wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na baadhi ya maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri za Mkoa wa Mara.
Wengine waliopo katika msafara huo ni wawakilishi wa Wizara ya Maji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Wizara ya Maliasili na Utalii, maafisa kutoka Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC).
Wengine walioshiriki maadhimisho haya ni maafisa kutoka mashirika yanayohusiana na uhifadhi katika Bonde la Mto Mara na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, baadhi ya wafanyabiashara, vikundi vya burudani na Waandishi wa Habari kutoa Mkoa wa Mara.
Ratiba ya maadhimisho haya iliyotolewa na Serikali ya Kenya inaonyesha kuwa ufunguzi rasmi wa maadhimisho haya ulifanyika tarehe 12 Septemba, 2024 na Gavana wa Jimbo la Narok huku shughuli za maonyesho ya bidhaa mbalimbali za wafanyabiashara na wajasiriamali, michezo na burudani, yanafanyika kuanzia Septemba 12 hadi tarehe 15 Septemba, 2024 ambayo ndio siku ya kilele.
Katika ufunguzi rasmi wa maonyesho haya, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dkt. Vincent Naano Anney aliyekuwa aliambatana na wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara.
Tarehe 13 Septemba, 2024 kulikuwa na shughuli za michezo, upandaji wa miti na shughuli za uhifadhi katika Msitu wa Mau uliopo katika eneo hilo huku maonyesho na michezo yakiendelea katika Mji wa Sekanani.
Leo tarehe 14 Septemba, 2024 shughuli za michezo na maonyesho zinaendelea katika Mji wa Sekanani huku Kongamano la Kisayansi kuhusu uhifadhi wa Mto Mara limefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara, katika Mji wa Narok.
Kesho tarehe 15 Septemba, 2024 kilele cha maadhimisho haya kinatarajiwa kutafanyika katika Mji wa Sekanani kwa shughuli za maonyesho ya biashara, burudani na mikutano ya hadhara.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya 13 ya Siku ya Mara ni Kwa Pamoja: Tuhifadhi Bonde la Mto Mara kwa Bioanuai Endelevu na Ustahimilivu wa Tabia nchi” yaani “Flowing Forward Together: Conserving the Mara Basin Ecosystem for Sustainable Biodiversity and Climate Resilience.”
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa