MTAMBI AONGOZA MJADALA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo ameongoza kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 na kuwataka washiriki kutoa maoni ili kuandaa dira hiyo itakayoliongoza Taifa kwa miaka 25 ijayo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amesema lengo la kikao hicho ni kutoa fursa kwa wananchi na viongozi wa Mkoa wa Mara kutoa maoni yao kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 ambayo ipo katika hatua za maandalizi.
“Dira inaonyesha matamanio na vipaumbele ya wananchi, Serikali na taasisi binafsi zinapotamani kufikia kwa muda flani na mipango mbalimbali inawekwa ili kufikia lengo hilo” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ulizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango April, 2024 Mkoani Dodoma wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni amezindua ushirikishwaji wa wadau wote kutoa maoni.
Kanali Mtambi amesema katika Mkoa wa Mara majadiliano hayo yamefanyika katika ngazi za Wilaya na leo yanahitimishwa katika ngazi ya Mkoa kabla ya maoni ya Mkoa wa Mara kuwasilishwa Tume ya Mipango kwa hatua zaidi.
Mhe. Mtambi amesema Tume ya Mipango imewasilisha katika Mkoa wa Mara maelekezo ya namna ya kukusanya maoni, mapendekezo na ushauri ili wananchi, viongozi na taasisi zitoe maoni kwa ajili ya dira mpya ya maendeleo ya Taifa kwa miaka 25 ijayo.
Mhe. Mtambi amesema kwa kawaida Nchi inakuwa na mipango ya muda mrefu, muda wa kati na muda mfupi na utekelezaji wake unaweza kulitoa Taifa kutoka katika eneo moja kwenda eneo jingine.
Kanali Mtambi amesema anatamani katika mipango ya miaka ijayo reli ya kisasa ya SGR iwe imefika Mkoa wa Mara kutokea Arusha au Mwanza ili kurahisisha usafiri kwa watu na mizigo kutoka katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Jumanne Sagini amesema Mkoa wa Mara umepiga hatua kubwa katika miundombinu ya barabara ambapo hapo awali wananchi wa Mkoa wa Mara walikuwa wanatumia zaidi usafiri kupitia nchi za Kenya na Uganda wakati wa kwenda Dar es Salaam na mikoa mingine.
Mhe. Sagini ameshauri Mkoa utilie mkazo kuhusu urejeshaji wa Bandari ya Musoma ili iweze kufanya kazi kuunganisha na treni ya SGR ambayo inatarajiwa kufika Mkoa wa Mwanza na hivyo bandari itasaidia katika usafirishaji wa mizigo na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa.
Mhe. Sagini amesema tayari Serikali imeshajenga meli nyingi na inaendelea kujenga nyingine na hivyo inawezekana bandari ya Musoma ikifufuliwa itasaidia katika kuimarisha usafiri wa mizigo na kuvutia wawekezajai zaidi katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Sagini amesema katika sekta ya elimu nchi imepiga hatua kubwa sana tumepanuka sana, walimu wapo wachache, walimu na wazazi tunaowajibu kuhakikisha wanafunzi wanasoma.
Tulikotoka ni mbali sana na tulipo sio kwamba tumefika bali tunaendelea kuboresha. Tujifunze kushukuru mambo yanayofanyika.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Mhe. Prof. Sospeter Muhongo amesema wakati Taifa linatoa maoni ni vizuri wataalamu wa mipango wakajiuliza wakati huo Dira inapotekelezwa Tanzania itakuwa na watu wangapi, dunia pia itaakuwa na watu wangapi ili kupanga mipango yenye uhalisia.
Prof. Muhongo amesema katika mwaka wa 2050 Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 120 hadi 141ambao ni zaidi ya mara mbili ya watu waliopo sasana mipango yote inatakiwa kuweka kwenye mahesabu watu hao ili Tanzania isipange mipango kwa ajili ya watu wachache wakati inakadiriwa kutakuwa na watu wengi.
Mhe. Muhongo amesema idadi ya watu ni muhimu kwa ajili ya kuangalia maendeleo tunayoyahitaji ni kwa ajili ya kuhudumia watu wangapi na kama mipango ya Taifa inaendana na idadi hiyo ya watu wanaotegemewa kuwepo wakati huo.
Ametolea mfano wa umeme na kusema kuwa kwa sasa umeme unatosheleza kwa kuwa bado idadi ya watu na viwanda na maofisi ni ndogo ukilinganisha na wakati huo na kutahadharisha kuwa ili kuwa na umeme wa uhakika wa wakati huo ni lazima kuangalia mahitaji halisi ya umeme kwa wakati huo na sio hali ya sasa hivi tu.
Aidha, washiriki wengi wamepongeza maendeleo yaliyofikiwa katika sekta mbalimbali hapa nchini na kuitaka Serikali kuendelea kuimarisha utendaji kazi katika utumishi wa umma ili maendeleo yaweze kufikiwa kiurahisi zaidi.
Awashiriki pia wamevipongeza vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa amani na utulivu uliopo nchini na kuvikata kurekebisha kasoro ndogo ndogo zinazovichafua vyombo hivyo.
Kikao hicho kimehusisha pia Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Taasisi za Umma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa